Repoti ya uchunguzi ya Pakistan yasema mauaji ya Sharif nchini Kenya 'yalipangwa'

Mwandishi hayati Arshad Sharif

Mauaji ya mwandishi wa habari za uchunguzi wa Pakistan nchini Kenya yalikuwa  “mauaji yaliyopangwa” timu ya wachunguzi wa Pakistani imesema katika ripoti iliyotolewa Jumatano.

Arshad Sharif, ambaye alikuwa analikosoa jeshi lenye nguvu nchini Pakistan, aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi akiwa ndani ya gari nje ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Polisi mjini Nairobi baadae walieleza masikitiko yao juu ya tukio hilo, wakisema lilifanyika kimakosa kwa wakati wakilisaka gari kama hilo lililokuwa limehusika na utekaji wa mtoto.

Mauaji ya Sharif yalipelekea shutuma kali na wito wa kufanyika uchunguzi huru.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alitangaza kuanzishwa uchunguzi na kuahidi kitakacho gunduliwa kitawekwa bayana kwa umma. Jeshi hilo na waandishi wa habari wa Pakistan pia walitaka uchunguzi ufanyike, kama ilivyokuwa kwa mjane wa Sharif, Javeria Siddique, na wanafamilia wengine.

Mwandishi huyo wa habari mwenye umri wa miaka 49 alikuwa anaishi nje ya nchi baada ya kukimbia nchini humo mwezi Agosti kuepuka kukamatwa akiwa anakabiliwa na kesi kadhaa, ikiwemo mashtaka ya uhaini, yaliyoelekezwa kwake kwa kutoa maoni katika kipindi chake kilichokuwa kinachukuliwa na jeshi kuwa kinawashambulia.

Wakati huo huo, polisi nchini Islamabad wamewafungulia mashtaka wafanyabiashara wawili wa Pakistani wanaoishi Kenya, ambao walikuwa ni wenyeji wa Sharif katika nchi hiyo ya Afrika, wakihusishwa na mauaji ya mwandishi huyo.

Maziko ya Arshad Sharif

‘ALIKUSUDIWA KUUWAWA’

Ripoti ya wachunguzi yenye kurasa 592, ambayo shirika la habari la AP imeiona, ilisema polisi ya Kenya imetoa taarifa zinazokinzana kufuatia mauaji hayo. Ikiwa ni sehemu ya uchunguzi huo, maafisa wawili wa Pakistan walisafiri kwenda Kenya ambapo walikutana na polisi na wenyeji waliompokea Sharif, ndugu wawili, Khurram na Waqar.

Kulingana na ripoti hiyo, Khurram aliwaambia wachunguzi alikuwa ndani ya gari pamoja na Sharif wakati wa tukio hilo la kupigwa risasi, wakisafiri kurudi nyumbani baada ya chakula cha usiku. Waliona kizuizi barabarani, ambacho Khurram aliamini kilikuwa kimewekwa na majambazi. Walipokipita kwa kasi, alisikia mlio wa risasi, alisema.

Khurram alisema baada ya hilo kutokea, alimpigia simu kaka yake ambaye alimshauri waendelee na safari mpaka wafike katika nyumba ya familia iliyoko shamba, kilomita kadhaa kutoka penye tukio. Walipowasili nyumbani, ndugu hao waligundua Sharif ameshakufa, Khurram alinukuliwa akisema hivyo.

Malcolm Webb wa Kituo cha televisheni cha Al Jazeera akiripoti kutoka eneo la tukio hilo la mauaji Kajiado Kenya, alisema ndugu hao hawajazungumza na vyombo vya habari tangu tukio hilo kutokea.

Lakini wakili wao anasema wawili hao “ hawahusiki na wao pia wanahofia maisha yao”, Webb alisema.

Ripoti hiyo ya uchunguzi haikutaja iwapo imegundua maelezo ya Khurram yana mashaka. Ilisema tu polisi wa Kenya kwa namna fulani “walitumika kama watekelezaji” wa mauaji hayo, pengine kwa kulipwa fedha au fidia – pia, bila ya kufafanua au kutoa ushahidi kuthibitisha tuhuma hizo.

Ripoti hiyo haikutoa ushahidi juu ya madai hayo na hapakuwa na maelezo ya haraka kutoka Kenya.

“Huu ulikuwa ni mpango uliolenga kuuwa … kinyume na tukio la makosa ya kufananisha” kama polisi wa Kenya wanavyodai, ripoti hiyo ilieleza. Ilijizuilia kumtuhumu mtu yeyote moja kwa moja, ikisema ni watu fulani fulani nchini Kenya, Dubai, na Pakistan wanaweza kuwa walihusika katika mauaji hayo.

Sharif alikuwa akiishi Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya kuondoka Pakistan mwezi Agosti na kabla ya kusafiri kwenda Kenya.

Ripoti hiyo ilipendekeza zaidi kuwa risasi iliyomjeruhi Sharif huenda ilifyatuliwa ndani ya gari au masafa ya karibu. Lakini haikufafanua.

Chanzo cha habari hii ni kituo cha televisheni cha AL JAZEERA na mashirika mengine ya habari