Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 02:56

Kenya: Taasisi huru yaanzisha uchunguzi wa haraka kufuatia kuuwawa Arshad Sharif


Arshad Sharif
Arshad Sharif

Mamlaka Huru ya Kutathimini Utendajikazi wa Polisi nchini Kenya, IPOA imeanzisha uchunguzi wa haraka kufuatia kitendo cha maafisa wa polisi katika kaunti ya Kajiado kumpiga risasi na kumuua mwanahabari maarufu wa Pakistani Arshad Sharif  Jumapili usiku.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amezungumza na Rais wa taifa hilo William Ruto kuhusu kifo cha mwanahabari huyo ambaye polisi nchini Kenya wanasema ni kisa kilichotokea kimakosa.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif

Halmashauri hiyo, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari jijini Nairobi, Jumatatu, imeeleza kuwa imewatuma wachunguzi wake katika jimbo la Kajiado kuchunguza mauaji ya mwanahabari huyo wa Pakistani.

Maafisa wa polisi nchini Kenya wanaeleza kuwa alimiminiwa risasi kimakosa, Jumapili usiku katika barabara ya Magadi-Kajiado baada ya kuvuka kizuizi kilichowekwa na maafisa wa polisi kudhibiti kisa cha wizi wa gari jijini Nairobi.

Anne Makori, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, amewaeleza wanahabari kuwa uchunguzi wa halmashauri hiyo utawekwa wazi na kupendekeza afisa wa polisi aliyehusika afunguliwa mashtaka kwa kosa hilo.

Idara ya polisi kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Jumatatu, mchana, imeeleza kuwa inajutia kisa hicho kilichotokana na kusambazwa kwa taarifa za wizi wa gari la polisi la Pangani lililokuwa limeibiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maafisa waliokuwa wakilifuata gari hilo kuelekea Magadi waliwatahadharisha wenzao huko Magadi ambao walilazimika kuweka kizuizi cha barabarani.

Hata hivyo, gari la Bw Sharif na nduguye Kurram Ahmed, lilivuka kizuizi hicho cha polisi baada ya kukaidi amri ya maafisa wa polisi na papo hapo kumfanya afisa wa polisi kufyatua risasi, na kumuua.

Gazeti la “Daily Nation” nchini Kenya, linaripoti kuwa maafisa wa polisi walilipiga risasi gari hilo kutoka pande zote na kuliacha likiwa na matundu tisa ya risasi upande wa kushoto wa kioo cha mbele, ambao ni upande aliokuwa ameketi Arshad Sharif.

Pia matundu mawili ya risasi yaliyopatikana kwenye skrini ya nyuma kushoto, tundu moja la risasi kwenye mlango wa nyuma wa kulia, matundu manne upande wa kulia wa buti na tairi moja la mbele la kulia ambalo lilikuwa limetobolewa na risasi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nduguye alimpata Arshad Sharif akiwa na jeraha la risasi kichwani, ambalo huenda ndilo lililomua, kwani risasi lilipenya nyuma ya kichwa chake na kutoka mbele, Daily Nation linaripoti.

Je, ni uchunguzi wa aina gani unastahili kufanyika wakati maafisa wa polisi wanakiri mauaji? George Musamali, Mtaalam wa usalama nchini Kenya anaeleza.

Aliongeza kudadisi, “Lakini, Je, mbona maafisa wa polisi wanafyatua risasi moja kwa moja bila kufuata utaratibu unaofaa? Bw Musamali alihoji.

Wakati mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti ya Chiromo jijini Nairobi, kuruhusu uchunguzi zaidi, Miungano ya waandishi wa habari imeshtumu tukio hilo na kutaka uchunguzi wa kina kufanyika kubaini kilichotokea na wahusika kufunguliwa mashtaka.

Mauaji ya Bw Sharif, yanajiri wakati nchini Kenya kuna mjadala mkali kutokana na kuvunjiliwa mbali kwa kikosi maalum cha polisi maarufu SSU kinachodaiwa kuhusika na msururu wa utekaji nyara, mateso na mauaji ya kiholela.

Kadhalika kuhusishwa na kutoweka kwa raia wawili wa India, Zaid Sami Kidwai na Zulfiqar Ahmad Khan wanaoripotiwa kuwasili nchini Kenya kusaidia kampeni za kisiasa za rais wa sasa William Ruto.

Wanaripotiwa kutoweka Julai na dereva wao Mkenya Nicodemus Mwania.

Waliokuwa wasimamizi wanne wa kikosi hicho cha polisi wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka Jumatatu jijini Nairobi, hatma yao itajulikana Jumatano baada ya maamuzi ya mahakama.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya.

XS
SM
MD
LG