Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:09

Jen. Muhoozi: Mimi sio mtoto, babangu hawezi kuniamrisha kutoandika kwenye Twitter


Generali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni Mei 25, 2016
Generali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni Mei 25, 2016

Mshauri wa ngazi ya juu kuhusu operesheni maalum wa rais wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kwamba hataacha kuandika ujumbe wenye utata kwenye mitandao ya kijamii na kwamba yeye si mtoto wa kuambiwa cha kufanya.

Hii ni baada ya watumiaji wa mtandao wa Twitter nchini Kenya kuandika wakisema kwamba rais Yoweri Museveni anastahili kumdhibithi mwanawe kuhusu mambo anayoandika kwenye Twitter na kwamba hayalingani na hadhi yake kama Jenerali katika jeshi la nchi.

“Nasikia kuna waandishi wa habari wa Kenya wamemwambia baba yangu kwamba anipige marufuku nisitumie mtandao wa Twitter,” ameandika Jenerali Muhoozi kwenye ukurasa wake, akiongezea kwamba “huo sio utani? Mimi ni mtu mzima na hakuna mtu yeyote anaweza kuniwekea marufuku ya kitu chochote.”

Ujumbe wa wakenya kwenye Twitter ulifuatana na swali la mwandishi wa habari wa televisheni ya Kenya kwa rais Yoweri Museveni kama anaweza kumdhibithi mwanawe kwenye mitandao ya kijamii, wakati wa mahojiano maalum.

“Kama Muhoozi angekuwa akiandika maswala kuhusu michezo, na mambo yasiyo na utata, isingekuwa shida yoyote lakini kuzungumzia nchi nyingine au siasa za Uganda, hilo lazima akome kufanya,” Museveni amesema.

Mara ya 4 Museveni amtaka mwanawe kuwa makini kwenye mitandao ya kijamiii

Hii ni mara ya nne mwaka huu, Museveni amemshauri mwanawe Muhoozi kuacha kuandika ujumbe wenye utata kwenye mitandao ya kijamii.

Wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Muhoozi, iliyofanyika katika ikulu ya rais ya Entebbe, rais Museveni na rais wa Rwanda Paul Kagame, walisema kwamba walikuwa wamshauri Muhoozi kuacha kuandika ujumbe wenye utata kwenye mitandao ya kijamii. Wakati huo alikuwa ameandika kuhusu vita vya Tigray, nchini Ethiopia.

Museveni pia alimshauri Muhoozi kujiepusha na kuandika ujumbe wenye utata kwenye mitandao ya kijamii wakati wa kikao cha maafisa wa ngazi ya juu wa usalama nchini Uganda, uliofanyika Kisoro, lakini hakuna mabadiliko.

Jenerali Muhoozi, anadai kwamba wafuasi wa babake, wakiwemo maafisa wa ngazi ya juu na ambao wamefaidika kutoka katika chama kinachotawala cha National Resistance Movement NRM, hawajawahi kumtetea anaposhambuliwa na watu kwenye mitandao ya kijamii na hivyo inabidi ajitetee mwenyewe.

Ujumbe wa Muhoozi unatatiza kazi ya wizara ya mambo ya nje

Maafisa katika wizara ya mambo ya nje ya Uganda wamekuwa wakisema kwamba kazi yao imekuwa ngumu kutekeleza kutokana na ujumbe wa mwanawe Museveni.

Lakini wafuasi wa Muhoozi wamekuwa wakisema kwamba alifanikiwa kurejesha uhusiano mwema kati ya Uganda na Rwanda bila kusaidiwa na wizara ya mambo ya nje na hivyo wanastahili kukoka kumkosoa.

Uhusiano kati ya Rwanda na Uganda ulikuwa mbaya kiasi cha Rwanda kufunga mpaka.

Wizara ya mambo ya nje ya Uganda imekuwa ikitoa taarifa kila mara Muhoozi anapoandika ujumbe wake, ikisema kwamba “ujumbe anaoandika kila mara ni mawazo yake ya binafsi na wala sio msimamo wa serikali.”

Muhoozi anapenda tabia ya Donald Trump

Jenerali Muhoozi anampenda sana aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump, na ametangaza hadharani kwamba anapenda namna alivyokuwa akitumia mtandao wa Twitter.

Ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter amesababisha hali ya sintofahamu ndani na nje ya Uganda.

Amekuwa akiandika namna Afrika inaiunga mkono Russia katika uvamizi wake Ukraine na kwamba yeyote anayeipinga Russia anaipinga Afrika.

Sheria za Uganda haziruhusu wanajeshi kuzungumzia hadharani maswala ya siasa, na wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakimtaja ajiuzulu na kushtakiwa.

XS
SM
MD
LG