Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:13

Ruto: Nipo tayari kufanya kazi na mpinzani wangu Kalonzo Musyoka


Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto) wakati huo akiwa waziri wa fedha, Aliyekuwa makam rais Kalonzo Musyoka (katikati) na rais wa sasa wa Kenya William Ruto (kulia) wakati huo akiwa amefutwa kazi kama waziri wa elimu ya juu. Aprili 11, 2011.
Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto) wakati huo akiwa waziri wa fedha, Aliyekuwa makam rais Kalonzo Musyoka (katikati) na rais wa sasa wa Kenya William Ruto (kulia) wakati huo akiwa amefutwa kazi kama waziri wa elimu ya juu. Aprili 11, 2011.

Rais wa Kenya Dr. William Ruto, amesema kwamba yupo tayari kufanya kazi na mmoja wa viogogo wa muungano wa Azimio Kalonzo Musyoka.

Akizunguza mjini Kilifi wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la Africa in-Land, Ruto amesema kwamba amekuwa akimtafuta kiongozi wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka, kufanya naye kazi serikalini.

Chama cha Wiper ni mojawapo ya vyama vinayounda muungano wa Azimio, wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

“Nipo tayari kufanya kazi na Kalonzo wakati wowote ule, atakapokuwa tayari,” amesema Ruto. Musyoka alikuwa makamu wa rais wakati wa utawala wa hayati Mwai Kibaki. Alikuwa pia waziri wa mazingira, mambo ya nje na elimu chini ya utawala wa hayati Daniel Arap Moi.

Ruto amesema kwamba yupo tayari kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni kwamba atafanya kazi na Kalonzo Musyoka, akiongezea kwamba Kalonzo ndiye amekuwa akitaka kufanya kazi na upinzani.

"Stephen ni ndugu yangu mkubwa na atakapokuwa tayari kufanya kazi na mimi, nitamkaribisha.”

"Nilipokuwa hapa wakati wa kampeni, niliwaambia kwamba kwa mapenzi ya mungu, nitakuwa rais na nitamshirikisha Stephen katika kuunda serikali. Ningependa kuwaambia kwamba mimi mwenyewe nilimtafuta na tukakaa chini, tukazungumza. Nilimuomba aungane na mimi lakini bado anataka kujaribu namna kazi ya upinzani inavyofanywa,” ameendelea kusema Ruto.

Akizungumza katika hafla hiyo, naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua, amesema kwamba hawana shida yoyote kufanya kazi ya serikali na kiongozi huyo wa chama cha Wiper. “Tatizo pekee ni kwamba hatumuelewi.”

Gavana wa Machakos, ambaye ni mwanachama wa ngazi ya juu katika chama cha Wiper Waninya Ndeti, naye amesema kwamba “hatuna shida na Kalonzo, tunamsubiri. Ni nyinyi mtakaoamua kile mnataka kufanya naye kwa sababu hata sisi hatumuelewi.”

Kuunda baraza la mawaziri la upinzani

Musyoka hata hivyo alisema siku chache zilizopita kwamba muungano wa Azimio, unajitayarisha kuunda baraza la mawaziri la upinzani ili kuhakikisha kwamba serikali inatekeleza majukumu yake vipasavyo.

Kalonzo alisema kwamba muungano wa Azimio utatangaza baraza hilo la mawaziri punde tu kiongozi wake Raila Odinga atakaporudi Kenya kutoka India.

Hakuna taarifa kuhusu ziara ya Odinga nchini India.

Musyoka amesema kwamba baraza hilo la mawaziri litakuwa na bajeti maalum ambayo itagharamiwa na serikali.

"Hii ndio nchi yetu ambayo tunaiita nyumbani. Hatuna kwingine pa kwenda. Lazima tushirikiane na kuhakikisha kwamba serikali inatumikia watu wake,” amesema Kalonzo, akiongezea kwamba upinzani utatekeleza wajibu wake vipasavyo.

“Na tunataka kumwambia rais kwamba asikasirike tunapotekeleza majukumu yetu.”

Baraza la mawaziri lililokuwa limetangazwa na Odinga

Raila Odinga alikuwa tayari ametangaza baraza lake la mawaziri miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu endapo angeshinda uchaguzi wa urais nchini Kenya.

  • Martha Karua - naibu rais na waziri wa katiba.
  • Kalonzo – mkuu wa baraza la mawaziri (waziri mkuu)
  • Aliyekuwa spika wa bunge la taifa Kenneth Marende – Spika wa Senate
  • Aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya – waziri wa fedha
  • Peter Munya waziri wa kilimo
  • Alaiyekuwa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho - waziri wa ardhi.

XS
SM
MD
LG