Habiba alikuwa habembelezeki, akilia kwa huzuni juu ya hatma ya mama yake, Hatemon Nesa mwenye umri wa miaka 27, na mdogo wake Umme Salima aliyekuwa na umri wa miaka mitano. Familia hiyo ilifahamishwa karibuni kuwa walikuwa katika boti chakavu ya mbao ambayo ingjni yake iliharibika katikati ya bahari, boti hiyo ilikuwa inaelekea Malaysia.
Wasafiri wapatao 200 waliokuwa ndani ya boti ambayo iliondoka Bangladesh Novemba 25, wote walikuwa wakimbizi Warohingya, waliishiwa maji na chakula wakiwa safarini.
Katika mahojiano kwa njia ya simu Begum ameiambia Sauti ya Amerika “ Nesa alituambia kuwa watu waliokuwa ndani ya boti walifariki kwa njaa na kiu pale boti ilipokuwa ikienda mrama. Nilikuwa na wasiwasi binti yangu na mjukuu wangu nao watafuatia.”
“ Nililia sana, lakini siyo mbele ya Habiba. Nilimwambia kuwa Allah atamuokoa mama yako na mdogo wako, niliendelea kusali. “
“Wakiwa umbali wa mamia ya kilomenta baharini, Nesa pia alikuwa amechoka lakini alijikaza kwa ajili ya mwanawe mdogo”
“Mara baada ya kugundua kuwa boti haikuwa inaelekea Malaysia, wanawake nikiwemo mimi tulianza kupatwa na wasiwasi”, Nesa aliiambia sauti ya Amerika kwa njia ya simu. “ wakati boti ilipobebwa na mawimbi na kurudishwa kwenye maji ya India watoto wengi wapatao 30 walianza kulia kwa njaa na kiu. Walipowaona watoto wao wanalia kwa maumivu , mama zao pia wakaanza kulia.
Nesa alijikaza kulia , akihofia kumtia wasiwasi Salima. “ nilimkumbatia mwanangu ambaye alikuwa hajisikii vizuri baada kumywesha maji ya chumvi. Nilimfariji , nikimwambia kuwa nina uhakika Allah atatufikisha kule tuendako.” Nesa alisema.
Nesa ni miongoni mwa wakimbizi wengine 740,000, Nesa alikimbilia Bangladesh mwaka 2017, baada ya msako mkali wa jeshi la Myanmar kwa jamii hiyo ya waislamu wa Rohingya walio wachache. Mume wake alimtelekeza mara baada ya kujifungua binti yao wa pili.