Nchi ya Gambia ilikata rufaa katika mahakama ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa hapo Jumatano kukataa juhudi za kisheria za Myanmar kumaliza kesi inayodai mauaji ya kimbari yaliyofanywa na nchi hiyo ya kusini-mashariki mwa Asia dhidi ya waislam walio wachache wa Rohingya.
Gambia iliwasilisha kesi hiyo mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki mwaka 2019 ikisema kwamba utawala wa Myanmar ulikiuka mkataba wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1948 wakati wa msako wa mwaka 2017 dhidi ya wa-Rohingya. Gambia inahoji ukandamizaji huo ulifikia mauaji ya kimbari na kwamba mahakama ya dunia lazima iiwajibishe Myanmar.
Wanajeshi wa Myanmar walianzisha kile walichokiita kampeni ya kuliondoa eneo la Rakhine kufuatia shambulizi la kundi la waasi la Rohingya. Vikosi vya usalama vilidaiwa kufanya ubakaji na mauaji makubwa na walichoma maelfu ya nyumba huku waislam wapatao 730,000 wa Rohingya wakikimbilia nchi jirani ya Bangladesh.
Jopo la kutafuta ukweli la Umoja wa Mataifa lilihitimisha kwamba vitendo vya mauaji ya kimbari vilifanywa wakati wa kampeni.