Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:36

UNHCR yapinga kuhamishwa kwa wakimbizi wa Rohingya


Wakimbizi wa Rohingya wakisafirishwa kuelekea n Bhashan Char. Desemba. 4, 2020. (AP Photo)
Wakimbizi wa Rohingya wakisafirishwa kuelekea n Bhashan Char. Desemba. 4, 2020. (AP Photo)

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa -UNHCR linasema linapinga kuhamishwa kwa wakimbizi wa Rohingya kutoka Cox Bazar, Bangladesh, kwenda kisiwa cha mbali katika Ghuba ya Bengal.

Mamlaka nchini Bangladeshi Ijumaa ilihamisha zaidi ya wakimbizi 1,500 wa Rohingya kwenda Bhasan Char, ghuba isiyo na wakazi ya kisiwa cha Bengal inayoweza kuathiriwa na vimbunga na kukabiliwa na mafuriko.

Msemaji Mkuu wa Ofisi ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa Babar Baloch anasema Umoja wa Mataifa haukuhusika katika kuandaa harakati hiyo. Anasema hakujua ni wakimbizi gani na alikuwa na habari chache sana juu ya operesheni ya jumla ya uhamishaji.

Anasema UNHCR ina wasiwasi kuwa wakimbizi wa Rohingya hawakuwa na taarifa waliyohitaji kufanya uamuzi huru na ulio na taarifa kamili juu ya kuhamia Bhasan Char.

“Tumesikia ripoti kutoka kwenye kambi kwamba baadhi ya wakimbizi wanaweza kuhisi wanashinikizwa kuhamia Bhasan Char au labda wamebadilisha maoni yao ya mwanzo juu ya kuhamishwa na hawataki tena kuhama. Ikiwa ni hivyo, wanapaswa kuruhusiwa kubaki katika kambi hizo.” Alisema Baloch.

Mwaka 2017, karibu wakimbizi milioni 1 walitoroka mateso na vurugu huko Myanmar na kwenda Cox's Bazar ambako wanaishi katika kambi duni zenye msongamano wa watu. Bangladesh inasema inataka kupunguza msongamano katika kambi hizo na inaona kuwahamisha hivi karibuni wakimbizi hao ni hatua ya kwanza katika mpango wa kuhamisha wakimbizi 100,000 kwenda Bhasan Char.

Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa serikali kuheshimu nia yake ya dhati kwamba harakati za kwenda katika kisiwa hicho zitakuwa ni za hiari. Baloch anasema UNHCR inasikitishwa na picha za wakimbizi walio na matatizo wakati wa mchakato wa kuhama na imepeleka wasiwasi wake kwa mamlaka za Bangladeshi.

“Tunasisitiza tena kwamba harakati zote za kuhama kama ilivyotajwa hapo awali kwa Bhasan Char lazima ziwe za hiari na kulingana na mashauriano na habari kamili juu ya hali ya Maisha katika kisiwa hicho na haki na huduma ambazo wakimbizi wataweza kupata.” Aliongeza Baloch.

Baloch anasema Umoja wa Mataifa una habari kidogo juu ya hali katika kisiwa hicho na inataka serikali itoe ruksa ya kutembelea kambi hizo ili kuhakikisha kuwa kisiwa hicho ni mahali salama pa kuishi. Anasema wakimbizi lazima wapate fursa ya kupewa huduma za afya, maisha na elimu na walindwe kutokana na majanga ya asili na hatari nyingine.

Imetayarishwa na Sunday Shomari, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG