Kupitia taarifa, Blinken amesema kwamba msaada huo ni pamoja na zaidi ya dola milioni 93 zitakazotolewa kupitia wizara yake, na nyingine milioni 77 kupitia shirika la misaada ya kimataifa la Marekani USAID. Amesema kwamba dola milioni 138 zitatumika kwenye program ya kufadhili jamii zilizotoa hifadhi kwa wakimbizi hao nchini Bangladesh.
Waziri huyo ameongeza kwamba msaada huo unafikisha karibu jumla ya dola bilioni 1.9 zilizotolewa na Marekani tangu 2017. Mapema mwaka huu Marekani ilitangaza kampeni dhidi ya watu wa Rohigya kuwa mauaji ya halaiki. Blinken amesema kwamba msaada huo utawasaidia zaidi ya wakimbizi 940,000 wa Rohingya, na wengine 540,000 waliotoa hifadhi kwao nchini Bangladesh. Baadhi ya misaada ni kama vile chakula, maji safi, dawa, makazi pamoja na elimu.