Wafuatiliaji wa haki za binadamu wameripoti kuwa mamia wamefariki, wakiwemo watoto, huku maandamano hayo yakiingia wiki ya tano.
Waandamanaji walipiga makelele “Uanguke utawala wa Dikteta” katika mitaa ya Ardabil huko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Nje ya vyuo vikuuu katika miji ya Kermanshah, Rasht na Tehran, wanafunzi waliandamana, kulingana na kanda za video zilibandikwa kwenye mitandao ya kijamii. Katika mji wa Sanandaj, kitovu cha maandamano katika mkoa wa kaskazini wa Kikurdi, wasichana wa shule walipiga kelele, “Mwanamke, maisha, uhuru,” katika mtaa wa katikati.
Maandamano hayo yalizuka kutokana na hasira za umma kufuatia kifo cha msichana wa miaka 22 Mahsa Amini aliyefariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Alikamatwa na polisi wa maadili wa Iran mjini Tehran kwa kukiuka kanuni ya mavazi yasiyokubalika katika Jamhuri ya Kiislam. Serikali ya Iran inasisitiza kuwa Amini hakutendewa vibaya wakati akiwa anashikiliwa na polisi, lakini familia yake inasema miwili wake ulionekana na alama za kupigwa baada ya kukamatwa na polisi.
Takriban waandamanaji 233 wameuawa tangu maandamano hayo kuikumba Iran Septemba 17, kulingana na kikundi kinachofuatilia haki za binadamu chenye makao yake nchini Marekani HRANA. Kikundi hicho kilisema 32 kati ya hao waliofariki walikuwa chini ya umri wa miaka 18. Kikundi cha Haki za Binadamu chenye makao yake Oslo kinakadiria kuwa watu 201 wameuawa.
Mamlaka nchini Iran zimekanusha kuwepo hali ya vurugu kama ilivyoelezwa na Magharibi, bila ya kutoa ushahidi wowote.
Hasira ya umma Iran imefungamana na kifo cha Amini, ikiwasukuma wasichana na wanawake kuvua hijab zao ambazo ni lazima kuzivaa wakiwa mitaani kuonyesha mshikamano wao. Maeneo mengine ya jamii, ikiwemo wafanyakazi na mafuta, pia wameungana na maandamano hayo, ambayo yameenea angalau katika miji 19, ikileta changamoto kubwa kabisa kwa utawala wa kidini tangu kuanza kwa harakati za Green Movement mwaka 2009 nchini humo.
Migomo ya kibiashara ilirejea tena Jumamosi katika miji mikubwa kote katika mkoa wa Kikurdi, ikiwemo Saqqez, nyumbani kwa Amini ambako maandamano yalianzia, Bukan na Sanandaj.
Serikali imejibu kwa msako mkali sana na kuwakamata wanaharakati na waandaaji wa maandamano hayo, ikiwakaripia wasanii wa Kiiran kwa uungaji mkono wao keaharakati hizo, hata kuwanyang’anya hati za kusafiria, na kutumia risasi za moto, gesi ya kutoa machozi na mabomu ya kelele kuwatawanya waandamanaji, ikipelekea vifo vya watu.
Katika kanda ya video iliyosambazwa Jumamosi, askari kanzu maarufu kama Basij, kikundi cha wanamgambo wa kujitolea, wanaonekana wakimlazimisha mwanamke kuingia ndani ya gari na wakifyatua risasi hewani katikati ya maandamano huko mjini Gohardasht, kaskazini ya Iran.
Kuzimwa kwa huduma ya intaneti imewawiya vigumu kwa waandamanaji kuwasiliana na ulimwengu, wakati mamlaka nchini Iran wamewakamata takriban waandishi wa habari 40 tangu kuanza ghasia hizo, kulingana na Kamati ya Kuwatetea Waandishi wa Habari.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AP