Maafisa wa Iran Jumatano wamesema watu watatu akiwemo afisa wa usalama waliuawa katika ghasia zilizoenea nchini humo, huku maandamano yenye hasira kutokana na kifo cha mwanamke aliyekuwa amewekwa mahabusu na polisi yakiendelea kwa siku ya tano mfululizo.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yameripoti kwamba mtu mmoja zaidi aliuawa Jumanne, naye kamanda wa polisi huko Kurdistan Ali Azadi ametangaza kifo cha mtu mwingine, kulingana na shirika la habari la Tasnim, na kufikisha idadi ya vifo kuwa nane.
Kifo kilichotokea wiki iliyopita cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22, ambaye alikamatwa na polisi wa maadili mjini Teheran “kwa mavazi yasiofaa” akikata kufunika kichwa, kiliibua hasira kali juu ya masuala mbalimbali ikiwemo uhuru katika taifa hilo la kiislamu na uchumi unaoyumba kutokana na vikwazo vya nchi za magharibi.
Baada ya kuanza kwa maandamano Jumamosi wakati wa mazishi ya Amini katika jimbo la Iran la Kurdistan, maandamano yalifanyika sehemu kubwa ya nchi, na kusababisha makabiliano huku vikosi vya usalama vikijaribu kuyazima.
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei hakutaja maandamano Jumatano katika hotuba yake alipokua anaadhimisha siku ya vita vya Iran na Iraq vya mwaka wa 1980 na 1988.