Shirika la habari la IRNA lilisema Jumapili kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iliwaita mabalozi wa Uingereza na Norway Jumamosi kuwasilisha madai yao kwa wajumbe hao.
Tehran ilitaja tabia ya uhasama ya vyombo vya habari vya lugha ya Kiajemi yenye makao yake mjini London, wakati ikimlalamikia mwanadiplomasia wa Norway kuhusu msimamo wa kuingilia kati wa spika wa bunge la nchi hiyo, ambaye ameelezea uungaji mkono wake kwa waandamanaji kwenye ujumbe waTwitter.
Maandamano yalizuka zaidi ya wiki moja iliyopita kote nchini Iran, huku waandamanaji wakikasirishwa na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22 wa Kikurdi, Mahsa Amini. Ni wimbi kubwa la maandamano kutokea dhidi ya serikali katika muda wa miaka mingi.
Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa kitaifa wa Rais wa Marekani Joe Biden, aliambia kipindi cha “This Week” cha ABC siku ya Jumapili kwamba maandamano ya Iran yanaonyesha imani iliyoenea kwamba waandamanaji wanastahili utu na haki zao na kwamba Marekani inawaunga mkono.
Alisema Marekani inaunga mkono watu wanaotetea haki zao.
Baadhi ya wanawake wa Iran wamekata nywele zao hadharani au kuchoma hijabu zao barabarani huku umati wa watu wenye hasira ukitoa wito wa kuangushwa kwa Kiongozi Mkuu wa kidini Ayatollah Ali Khamenei.
Televisheni ya taifa ya Iran inasema watu 41 wameuwawa kwenye ghasia za wiki moja. Serikali imefunga mawasiliano ya mtandao ili kuzuia habari kusamba na kuchochea ghasia zaidi mitaani.