Mpaka kufikia siku ya Ijumaa, vikundi vya kutetea haki za vyombo vya habari vinavyofuatilia kukamatwa kwa waandishi ambao walikuwa wanaripoti kifo cha Mahsa Amini, 22, na maandamano yanayoendelea wamerekodi kukamatwa kwa waandishi takriban 28.
“Katika mgogoro unaoendelea – maandamano kufuatia kifo cha Mahsa Amini – tumeshuhudia ukandamizaji ambao haujawahi kutokea kwa vyombo vya habari, na tunawaona wanawake ndio walengwa wakuu,” Kiran Nazish alisema, mkurugenzi muasisi wa Muungano wa Wanawake Walio Katika Uandishi wa Habari (CFWIJ), taasisi ya mashinani ambayo imejikita kuwatetea waandishi wanawake na LGBTQ.
Nazish aliiambia VOA kuwa licha ya CFWIJ kuweza kuthibitisha maeneo kadhaa wanayoshikiliwa waandishi, “ hatufahamu ni mamlaka zipi zimewakamata” waandishi wengine.
Nchini Iran, alisema, “ Waandishi wanafungwa jela na baadae kutoweka.”
Kamati ya Kutetea Waandishi wa Habari (CPJ) yenye makao yake New York, ambayo pia inafuatilia ukamataji huo, ilisema kuwa wengi wao wanachukuliwa kutoka majumbani mwao wakati wa usiku na maaskari ambao hawaonyeshi nyaraka zozote za mahakama au hati ya kuwakamata. Wengi waliokamatwa hawajafunguliwa mashtaka rasmi.