Hasira ya wanafunzi hao inatokana na kifo cha msichana kilichotokea akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Raisi alizungumza na wahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Alzahra mjini Tehran, wakiimba mashairi ambayo yaliwalinganisha “wanaofanya ghasia” na nzi, wakati maandamano nchi nzima yakiingia wiki ya nne.
“Wanafikiria wataweza kufanikisha malengo yao maovu katika vyuo vikuu,” Raisi alisema kupitia televisheni ya taifa. “Bila ya kufahamu, wanafunzi wetu na wahadhiri wako macho na hawataruhusu adui kufanikisha malengo yao maovu.”
Kanda ya video iliyobandikwa katika Twitter na wanaharakati wa 1500tasvir, tovuti iliyoonyesha kile ilichosema kuwa ni wanafunzi wa kike wakipiga kelele “Raisi ondoka” na “Viongozi wa dini ondokeni” wakati rais alipotembelea katika chuo chao. Kanda ya video nyingine iliyowekwa katika mitandao ya kijamii iliwaonyesha wanafunzi wakipiga kelele: “Hatumtaki mgeni fisadi,” wakikusudia ni Raisi.
Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha mara moja kuhusu kanda hiyo ya video.
Ripoti ya uchunguzi wa maiti ya serikali ilikanusha kuwa Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 alifariki kutokana na kipigo katika kichwa na viungo wakati akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa maadili na kukihusisha kifo chake na matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo, vyombo vya habari vya serikali vilisema Ijumaa.
Amini raia wa Iran mwenye asili ya Kikurdi alikamatwa mjini Tehran Septemba 13 kwa kuvaa “vazi lisilokubalika,” na alifariki siku tatu baadae.
Kifo chake kilichochea maandamano nchi nzima, ikibainisha changamoto kubwa sana kwa viongozi wa kidini wa Iran ambao wamekuwepo madarakani kwa miaka kadhaa.
Wanawake walivua hijabu zao wakikaidi amri ya utawala wa kidini wakati umati wenye hasira ulipaza sauti wakiutaka utawala wa Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei uangushwe.
Serikali imeeleza kuwa maandamano ni njama ya maadui wa Iran ikiwemo Marekani, ikiwashutumu waasi wenye silaha – kati ya wengine – kusababisha uvunjifu wa amani ambapo takriban wanajeshi 20 wa vikosi vya usalama wameripotiwa kuuwawa.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters