Kiongozi wa jeshi asema Suu Kyi karibuni atafikishwa mahakamani

FILE - Waandamanaji wakishinikiza kuachiwa kwa kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi May 20, 2021.

Kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Myanmar Min Aung Hlaing amesema kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi yuko na afya njema nyumbani kwake na atafikishwa mahakamani siku chache zijazo, alisema hayo katika mahojiano ya kwanza tangu mapinduzi ya Februari 1.

Mapinduzi hayo yameitumbukiza nchi ya hiyo ya Asia Kusini Mashariki katika vurugu.

Kundi la kikabila lenye silaha linalopinga utawala katika mji wa kaskazini magharibi unaochimba madini ya jade Jumamosi walishambulia kituo cha kijeshi huku matukio mengine yakiripotiwa katika sehemu nyingine za Myanmar, vyombo vya habari vilisema.

Suu Kyi, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mapambano yake ya muda mrefu dhidi ya watawala wa zamani wa kijeshi, ni miongoni mwa watu zaidi ya 4,000 walioshikiliwa tangu mapinduzi hayo.

Anakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwa ni pamoja na lile la kumiliki redio za walkie-talkie kinyume cha sheria na kukiuka sheria ya siri za serikali.

"Daw Aung San Suu Kyi ana afya njema. Yuko nyumbani kwake na mzima wa afya. Atafikishwa mahakamani siku chache kujibu kesi," Min Aung Hlaing alisema kwa njia ya video akizungumza na mtangazaji wa lugha ya Kichina anayeishi Hong Kong kwenye Televisheni ya Phoenix Mei 20, na kurushwa leo Jumamosi.