Maafisa wa biashara kutoka nchi hizo mbili walifanya mazungumzo ya pande mbili Arusha, mwezi Aprili, kujaribu kutatua masuala kadhaa yenye utata ya kibiashara, ikiwemo kanuni za asili zilizoko kwa ajili ya baadhi ya bidhaa na utilianaji mashaka wa ubora wa bidhaa ambazo zinauzwa katika mipaka ya pande zote mbili.
Watu ambao wanafahamu mazungumzo hayo wameliambia gazeti la The East African kuwa mkutano wa kwanza baina ya pande hizo mbili ulifanyika Septemba 2017 na mkutano mwengine umepangwa kufanyika Mombasa mapema Julai 2019.
Mpaka sasa maafisa wa biashara wamefanya mikutano mitano ya pamoja baina ya nchi hizo mbili tangu 2017.
Mkutano hiyo inafuatia maelekezo yaliyotolewa na Wakuu wa Nchi mwezi Machi yakiwataka mawaziri wa biashara na wa masuala ya Afrika Mashariki kutoka Kenya na Tanzania kutatua vikwazo ambavyo havihusiani na ushuru ambavyo vinaathiri biashara kati ya nchi hizo mbili.
“Timu zetu za biashara zimekuwa zikikutana kwa sababu tunataka kutatua masuala haya kwa utaratibu mzuri,” amesema Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki Adan Mohamed.