Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:15

Marais kujadili pendekezo la muundo wa serikali kuu EAC


Baadhi ya marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Baadhi ya marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mkutano wa 20 wa Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika kesho Arusha, Tanzania, baada ya kuahirishwa mara mbili mwezi Novemba na Disemba 2018.

Masuala kadhaa ikiwemo uwezekano wa kuwa na serikali kuu inayo zijumuisha nchi 6 wanachama yatazungumziwa kwenye kikao hicho.

Chanzo kutoka ofisi ya katibu mkuu wa EAC kinasema Marais wa Tanzania, Uganda, Kenya na Rwanda wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa juu wa viongozi hao wa Afrika Mashariki.

Burundi itawakilishwa na makamu wa Rais Gaston Sindimwo ambaye tayari amekwisha wasili mjini Arusha. Sudan Kusini itawakilishwa na Waziri wa Biashara.

Ratiba inaonyesha masuala ambayo yatajadiliwa na viongozi hao ni pamoja na taarifa juu ya maendeleo ya ripoti inayohusu uundwaji wa serikali kuu ya nchi 6 wanachama wa EAC.

Ripoti inayohusu kurahisisha uundwaji wa viwanda vya kutengeneza nguo na viatu, ili wananchi wa mataifa waweze kupata bidhaa hizo kwa bei nafuu, pia watajadili utaratibu wa kuwepo katika EAC kiwanda kikubwa cha kuunganisha magari ili kupunguza gharama za kuagiza magari yaliotumika.

Suala la kuwepo mkataba wa soko huria kati ya EAC na Umoja wa Ulaya litajadiliwa pia kwenye mkutano huo, bila kusahau suala la michango ya nchi wanachama, ikifahamika kwamba kuna baadhi ya nchi kama Burundi na Sudan kusini ambazo zina malimbikizo ya michango.

Viongozi hao watazungumzia pia uwezekano wa kuikubalia Somalia kuwa nchi mwanachama.

Chanzo hicho kimeendelea kusema kuwa, pendekezo la Burundi la kuwataka marais kujadili mzozo kati ya Burundi na Rwanda halipo kwenye ajenda ya kikao hicho. Marais wanatazamiwa pia kujadili ripoti ya rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye ni msuluhishi katika mgogoro wa Burundi.

Rais Yoweri Museveni ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano wa marais wa jumuiya hiyo anatazamiwa kumkabidhi uongozi wa umoja huo kwa rais mwengine. Mwaka huu ni zamu ya Rais wa Rwanda kuchukuwa uenyekiti, lakini taarifa zinasema Rais Paul Kagame amesema hayuko tayari kuongoza mkutano wa marais kutokana na shughuli nyingi alizonazo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG