Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 20:52

Mawakili wataka EAC kuingilia kati mgogoro wa Uganda


Mke wa nyota wa muziki Kyagulanyi na wakili Asuman Basalirwa wakijaribu kupata ruhusa ya kuingia katika mahakama ya kijeshi kusikiliza kesi ya mbunge Kyagulanyi Ssentamu katika mji wa Gulu, Kaskazini mwa Uganda, Agosti 16, 2018.
Mke wa nyota wa muziki Kyagulanyi na wakili Asuman Basalirwa wakijaribu kupata ruhusa ya kuingia katika mahakama ya kijeshi kusikiliza kesi ya mbunge Kyagulanyi Ssentamu katika mji wa Gulu, Kaskazini mwa Uganda, Agosti 16, 2018.

Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yametakiwa kuingilia kati ili kusitisha ukiukaji wa haki za kibinadamu unaoripotiwa kuendelea kushuhudiwa nchini uganda tangu kukamtwa kwa wabunge, akiwemo Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Chama cha mawakili nchini Kenya, pamoja na Tume ya Kutetea Haki za Binadamu, wameelezea kusikishwa na jinsi wananchi wa Uganda wanavyo dhalilishwa na serikali hiyo huku wanahabari wakikandamizwa kwa kufanya kazi yao.

Kenya

Mawakili wa Kenya wamesema kwamba wataisitaki serikali ya Uganda katika mahakama ya Afrika Mashariki kwa kukiuka haki za binadamu.

Mashirika hayo yamesema machafuko ambayo yanashuhudiwa nchini Uganda yanamadhara makubwa kwa mataifa jirani hasa Kenya, na ni lazima yasitishwe.

Wakizungumza na wanahabari jijini Nairobi wakiwa wamefunga utepe wa rangi nyekundu kama ishara ya umoja na na raia wa Uganda, wakuu wa mashirika hayo wameitaka serikali ya Uganda kumwachilia huru Mbunge Robert Kyagulanyi na kusema kuwa kushikiliwa kwake na kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi ni dhulma kubwa.

“Sisi kama wanasheria wa Wakenya, na watu ambao wanapigania haki za binadamu na kutetea uhuru wa waandishi wa habari, tunataka serikali ya Uganda itimize jukumu lake la kuheshimu haki za kibinadamu.

Serikali ya Uganda inastahili kuruhusu Bobi Wine atibiwe na daktari wake, aachiliwe huru na wengine wote walio kamatwa wapewe haki. Tunataka serikali za Kenya, Tanzania na serikali zote katika jumuiya ya Afrika mashariki, zishurutishe utawala wa Uganda kuheshimu haki za kibinadamu” amesema Charls Kanjama, mwanachama wa chama cha mawakili nchini Kenya.

Mashirika hayo vile vile yanaitaka serikali ya Uganda kuheshimu uhuru wa kuongea, uhuru wa wandishi wa habari na vilevile kuanzisha uchunguzi jinsi dereva wa Bobi Wine alivyouwawa .

“Tuna watangazia Wakenya kwamba kwa muda wa wiki moja, tutakuwa tunavaa utepe mwekundu kortini au kwa kufunga kichwani ili kuonyesha kwamba tunaungana na Bobi Wine na wenzake ambao wamedhulumiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa sababu ya kutetea haki zao za kisiasa na uhuru wa kuongea. Kama Waafrika, hatutakaa kimya wakati wenzatu wanadhulumiwa katika nchi jirani” ameendelea kusema Charles Kanjama.

Mashirika hayo pamoja na mashirika mengine hapo kesho yanatarajiwa kushiriki maandamano kuonyesha umoja wao na wadhiriwa wa machafuko ambayo yanaendelea kushuhudiwa nchini uganda.

Wasanii nchini Kenya wakiwemo wanamziki maarufu Sauti Sol, nao wamepanga maandamano makubwa katika jiji la Nairobi, wakitaka Bobi Wine kuachiliwa huru.

Uganda

Nchini Uganda muungano wa kutetea haki za waandishi wa habari (HRNJ), umetoa muda wa saa 48 kwa jeshi la nchi hiyo UPDF kuwakamata maafisa wote wa jeshi walio rekodiwa wakiwapiga fimbo waandishi wa habari, la sivyo wataanza mgomo wa kutoandika habari kuhusu idara zote za usalama.

HRNJ inawataka UPDF kutaja majina ya maafisa wake waliohusika katika dhulma dhidi ya waandishi wa habari, na wafunguliwe mashtaka mbele ya umma.

Kiongozi wa HRNJ Robert Sempala, amesema kwamba msamaha uliotolewa na Mkuu wa Jeshi Generali David Muhoozi hauna maana iwapo maafisa waliohusika hawatashitakiwa.

“imekuwa kama mazoea kwa viongozi wa jeshi la UPDF kuomba msamaha baada ya kuwadhulumu waandishi wa habari, na baadaye kurudia dhuluma hizo hizo baada ya muda mfupi,” amesema Sempala.

Naibu Spika wa Bunge la Uganda

Kinyume na ripoti ya msemaji wa jeshi la UPDF Brigedia Richard Karemire kwamba mbunge Bobi Wine anayezuiliwa katika makao ya jeshi huko Makindye jijini Kampala, kwamba hana tatizo lolote la kiafya, naibu spika wa Bunge la Uganda Jacob Oulanya amepinga taarifa hiyo.

Amewaambia waandishi wa habari jijini Kampala kwamba mbunge huyo, pamoja na mwenzake Francis Zaake wanamaumivu makali sana na kwamba hali yao ya afya sio nzuri.

“kile nilicho kiona ni kwamba wote wawili wanahisi maumivu makali. Bobi Wine aliweza kuketi na tukazungumza. Tumefanyiana utani na tukacheka kidogo lakini anahisi maumivu makali,” Oulanya amenukuliwa na shirika la habari la Chimp reports baada ya kumtembelea mbunge huyo katika gereza la kijeshi la Makindye.

“Pia nimemtembelea Francis Zaake, naye anahisi maumivu makali. Ana vidonda kwenye viganja vya mkono” ameongeza naibu wa spika Jacob Oulanya.

“Wamefanyiwa ukaguzi wa viungo vya ndani ya mwili. Majeraha waliokuwa nayo ni ya nje ya mwili kutokana na kile walichosema ni kupigwa sana na maafisa wa jeshi,” amesema Oulanya.

Hatma ya Bobi Wine

Bobi Wine, anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya kijeshi kesho Alhamisi wakati kesi dhidi yake ya kutaka kuipindua serikali ya Rais Yoweri Museveni itakapoanza rasmi kusikilizwa.

Bobi wine na watu wengine 35 walikamatwa wiki iliyopita baada ya kutokea vurugu siku ya mwisho ya kampeni katika uchaguzi mdogo wa Manispaa ya Arua yaliyoacha mtu mmoja ameuwawa kwa kupigwa risasi na ikulu ya rais kudai kwamba gari la rais Museveni lilipigwa mawe na kupasuliwa kioo.

Imetayarishwa na waandishi wetu Hubba Abdi, Kenya na Kennes Bwire, Washinton DC.

XS
SM
MD
LG