Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 00:14

Wavuvi 109 kutoka Tanzania washikiliwa Kenya


Ramani ya Tanzania
Ramani ya Tanzania

Serikali ya Kenya inasema kwamba wavuvi 109 kutoka Tanzania, waliokamatwa katika bahari Hindi, waliingia maji ya Kenya bila idhini na walivunja shera za uhamiaji pamoja na kanuni za uvuvi.

Joseph Biwott, naibu wa mkuu wa kaunti ya Kwale nchini Kenya, ameeleza Sauti ya Amerika kwamba licha ya wavuvi hao kujua mpaka kati ya Kenya na Tanzania, walikaidi sheria na kuingia Kenya.

“Kulingana na sheria zetu za uvuvi, ili uvue samaki baharini, ni lazima uwe na kitambulisho kuthibitisha kwamba wewe ni raia wa Kenya na umesajiliwa kuvua katika maji ya Kenya. Hata Wakenya ambao hawana idhini ya kuvua samaki, huwa tunawakamata. raia hao wa Tanzania hawakuwa na stakabadhi yoyote.” ameeleza bwana Biwott.

Biwott, ameeleza kwamba kukamatwa kwao inatokana na hatua ya kila mara ya serikali ya Tanzania kuwakamata wakenya wanaovuka mpaka na kuingia Tanzania, na hivyo kuonekana kama hatua ya kulipiza kisasi.

“Watu hawa wanaishi kama watu wa jamii moja na hata wanazungumza lugha moja. Hata wanajua mpaka vizuri sana lakini huwa wanafanya shughuli zao kama jamii moja. Lakini serikali ya Tanzania imekuwa ikiwakamata wakenya kwa msingi kwamba wamevuka mpaka. Tuna orodha ya waliokamatwa hadi sasa. Maafisa wa polisi wa Kenya wamekuwa hawakamati raia wa Tanzania. Kwa hivyo, kuna mfumo mpya ambao nasi tunachukua kuimarisha usalama wetu” amesema Josephat Biwott.

Utawala wa kaunti hiyo sasa unataka viongozi kutoka Tanzania kukutana na wenzao wa Kenya ili kukubaliana kwamba visa vya kuwakamata raia wa nchi hizo mbili wanaoishi mpakani, vinakomeshwa.

“Kama viongozi wa Kwale, tunapanga kukutana na wenzetu wa Mkinga, Tanzania, tukutanena wenzetu kutoka wilaya ya Mkinga, Tanzania, wiki ijayo Jumatano, utakaohusishwa maafisa wa jeshi la majini kutoka nchi zote mbili, ili tumalize uhasama unaojitokeza”ameendelea kueleza Biwott.

Wavuvi hao 109 wa Tanzania walikamatwa katika eneo la Shimoni, kusini mashariki mwa bahari ya Hindi nchini Kenya karibu na mpaka na Tanzania.

Wamefikishwa katika mahakama ya serikali ya kaunti ya Kwale na kusomewa mashitaki ya kuingia nchini Kenya bila kibali, pamoja na kufanya shughuli za uvuvi katika maji ya Kenya bila idhini.

Hadi sasa, wavuvi 50 wameachiliwa kwa dhamana ya dola 200, huku 59 wakisalia korokoroni kwa kukosa kiasi hicho cha pesa.

“wamekuwa na harambee hapa,wakiongozwa na diwani wa Tanga. Wamefanya mchango na kutoa baadhi yao”.

Katika mahojiano ya simu, Waziri msaidizi wa uvuvi wa Tanzania Abdallah Hamis Ulega, ameambia sauti ya amerika kwamba wizara yake haijajua kama waliokamtwa walivunja sheria au la.

Amesema kwamba kama wavuvi hao walikamatwa wakiwa na samaki ndani ya maji ya wenyewe, basi walivunja sheria na kama wamevunja sheria, kile serikali ya Tanzania inaweza kufanya ni kuruhusu mamlaka kushughulikia swala hilo.

“kile ambacho ninaweza nikasema kwa kifupi ni kwamba jambo hilo kwa sasa, linashughulikiwa na serikali” amesema waziri msaidizi wa uvuvi wa Tanzania Abdallah Ulega.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC

XS
SM
MD
LG