Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 02:56

Wataalam waeleza athari za Tanzania kuzuia uchapishaji wa ripoti ya IMF


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Hatua ya serikali ya Tanzania kukataa uchapishaji wa Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Fedha Duniani, IMF, imekosolewa na wachumi wakisema itaathiri uwekezaji na ufadhili kwa nchi hiyo.

Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine inaonyesha kuwa ukuaji wa uchumi utapungua kasi mwaka 2019, kufikia asilimia 4 kutoka kiwango kilichokuwa kimekadiriwa cha asilimia 6.6 mwaka 2018.

IMF imesema kuwa uchumi wa Tanzania unaharibiwa na sera za serikali zisizotabirika na zinazoingilia kati maamuzi” katika ripoti yake ambayo imezuiliwa kuchapishwa na nchi hiyo.

Imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania umeyumba kutokana na sera za maamuzi kadhaa yaliyofanywa na uongozi wa Rais Magufuli.

Tanzania ilikataa kuruhusu ripoti hiyo kuchapishwa, IMF imesema Jumatano katika tamko lililowekwa kwenye tovuti yao. IMF imesema kuwa juhudi za kumtafuta msemaji wa serikali Hassan Abbasi ziligonga ukuta, kwani hakupokea simu yake.

“Itakuwa gharama kubwa sana kwa Tanzania, kuweza kufikia masoko ya kimataifa, hasa ukizingatia ilikuwa tayari ni vigumu kwao kupata ufadhili kutoka kwa mashirika ya kimataifa na kutoka kwa nchi wanazoshirikiana nazo baada ya baadhi ya sera za serikali kuanza kutekelezwa Septemba 2018,” amesema Jibran Qureishi, Mchumi wa kikanda wa benki ya Stanbic Holdings Plc, Nairobi, Kenya, akieleza hisia zake baada ya ripoti hiyo kuzuiliwa kuchapiswha na serikali ya Tanzania.

Madhara mengine yanayoweza kuikumba nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa Afrika Mashariki, ni kuwa nyuma au kupiga hatua ndogo katika kuboresha udhibiti wa matumizi yake” na kukurupuka katika vitega uchumi vya umma ambavyo havitakuwa na tija ya kiwango cha juu, kwa mujibu wa nakala ya ripoti ya IMF.

Uwekezaji wa kigeni umeshuka kwa asilimia 2 katika ukuaji wa kichumi wa taifa hilo 2017, kutoka asilimia 5, 2014, kwa mujibu wa benki ya dunia.

Hata hivyo makadirio hayo yalikuwa tofauti na yale yaliotolewa na serikali kwamba uchumi utakua kwa asilimia 7.3 mwaka 2019.

Msemaji wa Wizara ya Fedha nchini Tanzania hakutoa tamko lolote kufuatia ombi la shirika la habari la Reuters akidai kwamba alikuwa katika mkutano.

Ripoti ilichopishwa na Shirika la habari la Bloomberg ambalo limebobea katika kuandika masuala ya kiuchumi na fedha limesema kuwa pamoja na Rais John Magufuli kupata sifa kubwa ya kupambana na ufisadi na uzorotaji wa shughuli za serikali, lakini pia amekabiliwa na ukosoaji kwa sera zake ambazo wawekezaji wanasema zitaathiri vibaya nchi ya nne duniani kwa utoaji wa dhahabu.

Kwa mujibu wa kifungu cha nne cha mkataba wake na mataifa mbalimbali, IMF inaruhusiwa kuchunguza uchumi , hali ya kifedha na sera ya ubadilishanaji wa fedha ya wanachama wake ili kuhakikisha kuwa mfumo wake wa kifedha unatekelezwa bila matatizo yoyote.

Hatua hiyo inashirikisha ziara ya maafisa wa IMF ya kila mwaka katika taifa hilo ili kuangazia data mbalimbali na kufanya vikao na serikali pamoja na maafisa wa benki kuu.

Katika kipindi cha uongozi wake, serikali imewatia jela wawakilishi wa madini na makampuni ya simu ambayo yamekuwa na mivutano na serikali na kudai kuwa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Acacia Mining Plc ilipe kodi ya dola za Marekani bilioni 190, ikiwa sawa na kodi ya mapato ya miaka 200. Kampuni hiyo inamilikiwa na Barrick Gold Corp, iko katika mazungumzo kutafuta suluhu juu ya mgogoro huo.

XS
SM
MD
LG