Januari 30, kampuni hiyo Indo Power Solutions ililishangaza soko ilipojitokeza kununua, biashara yenye thamani kubwa katika soko, ya tani 100,000 za korosho kutoka serikali ya Tanzania baada ya makampuni maarufu ya kigeni kukataa kununua korosho hizo zikielezea bei anayoshinikiza Rais Magufuli hailipi.
Gazeti la The Sunday Nation limeripoti hayo Jumapili likieleza kuwa hivi sasa kampuni hiyo imekuwa ikimulikwa na mkurugenzi mtendaji wake Brian Mutembei, ambaye alisema wao ni “kampuni ya kununua bidhaa” inayoshughulika na zao la kahawa na biashara ya kuku, uagizaji wa vilevi na uuzaji wa bidhaa zinazotokana na petrol.
Hii imefuatia hatua ya Tanzania kuachana nao mwezi Machi kwa kushindwa kufanya malipo.
“Achana na kampuni hiyo ambayo ilisaini mkataba na sisi mjini Arusha. Wameshindwa kutekeleza masharti ya mkataba huo na ilibidi tuachane nao,” Joseph Kakunda, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Tanzania ameliambia gazeti la Sunday Nation.
Wakati huo maafisa walipokuwa wanasaini mkataba huo na kampuni ya Indo Power, wachambuzi wa mambo ya biashara walikuwa tayari wanaeleza wasiwasi wao juu ya uwezo wa kampuni hiyo kutekeleza manunuzi hayo, ilivyokuwa ni kampuni haifahamiki kujishughulisha na mchakato au biashara ya korosho.
Katika mkataba huo, ilikuwa imeahidi kutuma dola za Marekani milioni 180 (Shilingi milioni 18) kwa ajili ya manunuzi ya korosho “katika kipindi cha siku tatu”, na kusababisha mkataba huo kutiliwa wasiwasi.
“Walitakiwa kuwa wamelipa malipo kamili katika kipindi cha miezi miwili kulingana na mkataba huo uliosainiwa. Lakini kampuni hiyo ilivunja masharti na kanuni za mkataba na imeondolewa,” amesema Kakunda.
Tanzania imeanza sasa kuandaa mpango mwengine, ikiorodhesha makampuni sita kuweza kununua korosho hizo, mbili kati ya hizo ni za wazawa.
“Kampuni hizi sita mpya ziko hivi sasa katika mchakato wa kutekeleza maelekezo ya mkataba. Zile ambazo zitafanya malipo mwanzo ndizo zitaweza kununua korosho hizo,” Kakunda amesema.
Juhudi za kumtafuta Mutembei zilikuwa zimegonga ukuta baada ya kumpigia simu mara kadhaa naye hakujibu. Lakini katika duru za wafanyabiashara Kenya, Mutembei anajulikana kuishi maisha ya kifahari akiwa mara nyingi na viongozi maarufu katika ngazi za kisiasa.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.