Sikitiko la wakulima
Katika Mji wa Nanyamba, na Masasi Mtwara, kusini mwa Tanzania, wananchi wanaeleza kuwa kuchelewa kwa malipo ya korosho walizouza kunawaathiri pakubwa hasa katika msimu huu wa kuanza kwa masomo ya watoto wao.
Shughuli ya ununuzi wa korosho inayofanywa na serikali nchini Tanzania bado inaendelea huku hali ya mambo ikionekana kuwa tata kutokana na uwepo wa malalamiko toka kwa wakulima hasa juu ya ucheleweshwaji wamalipo yao.
Tamko la Waziri wa Kilimo
Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Kilimo, Japhet Hasunga, anaeleza kuwa kuchelewa kwa malipo ya baadhi ya wakulima ni kutokana na uhakikina changamoto kadhaa ikiwemo kasoro katika taarifa za kibenk za wakulima.
Kauli ya Waziri Mkuu
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa anasisitiza kuwashughuli ya uhakiki wa wakulima na mazao ni lazima ifanyike ili kuwabaini wanaojaribu kudanganya.
Wasemavyo wataalam
Kwa mujibu wa taarifa ya timu ya wataalamu inayohusika na utekelezaji wa operesheni korosho zoezi la ubanguaji korosho linaweza kuchukua hadi miezi 14 kubangua korosho za msimu wa mwaka 2018/19 zinazofikia tani laki 2 na 75 elfu, na hii nikutokana na viwanda vingi kutofanya kazi hivi sasa.
Hata hivyo serikali nchini humo imechukuwa hatua ya kuwaita tena mezani wafanyabiashara wanaotaka kubangua korosho zilizokusanywa. Serikali imekaririwa na vyombo vya habari ikiwaalika tena wafanyabiashara wa korosho ambao wanataka kununua korosho na kuzibangua wenyewe kufanya hivyo
Serikali ya Tanzania ilitangaza mwaka 2018 mwishoni uamuzi wake wa kununua korosho kutoka kwa wakulima baada ya kuibuka mzozo wa ununuzi wa zao hilo kwa bei elekezi ya shilingi elfu tatu kwa kilo.