Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:00

Wabunge wadai urasimu unawakimbiza wawekezaji Tanzania


Waziri Mwijage
Waziri Mwijage

Wabunge nchini Tanzania wamesisitiza kuwekwa utaratibu usio na urasimu kwa wawekezaji kutokana na utaratibu wa sasa kuwa na vikwazo vingi vinavyokimbiza wawekezaji.

Aidha, wabunge hao wameishauri serikali kutumia vyema rasilimali na malighafi zilizopo katika kuijenga sekta hiyo ya viwanda.

Wametaka kuwa mafanikio ya viwanda hivyo yasiishie tu kwenye kuongeza ajira bali kuinua uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Pamoja na hayo, wabunge hao, wameitaka Serikali kuanzisha kituo kimoja kwa ajili ya kutoa huduma zote katika sehemu moja kwa wawekezaji jambo litakaloongeza vivutio kwa uwekezaji lakini pia kuwarahisishia wawekezaji hao kufanikisha kiurahisi taratibu za kuwekeza nchini.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema ni wakati sasa kwa serikali kuondoa vikwazo vyote vya uwekezaji ili kutimia ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Kauli hiyo Bashe aliitoa wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliyowasilishwa juzi na waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage,

Alitoa mfano wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania iliyotolewa Aprili, mwaka huu inayobainisha kuwa uzalishaji viwandani umeshuka kutoka dola za Marekani milioni 1.4 mpaka dola za Marekani 870,000, usafirishaji bidhaa nje umeshuka kwa dola za Marekani milioni 80, bidhaa za samaki dola za Marekani milioni 20 na usafiri na mawasiliano -21.6.

Mbunge huyo alisema usafirshaji wa bidhaa za mazao ya asili nao ulishuka bidhaa pekee iliyokuwa ni korosho kutokana na kuongezeka kwa bei, tumbaku imeshuka kutoka Dola za Marekani milioni 343 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 281 mwaka huu, pamba imeshuka kwa Dola za Marekani milioni 10, kahawa Dola za Marekani milioni tisa na karafuu kwa Dola za Marekani milioni 13.

Tatizo ni sera za kodi kutotabilika, “sheria ya uwekezaji kifungu namba 19 tumeibadilisha mwaka 2009 kwa kuifuta, tukaibadilisha mwaka 2010, 2012, 2014 na 2015 tunafuta na kuruidisha wakati ni nchi moja, tunakimbiza wawekezaji kwa kuwa hatutabiriki,” alifafanua.

Alisema pia kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia mazingira ya uwekezaji nchini ni magumu, kwani ili uwe na kiwanda cha maziwa lazima uwe na nyaraka zaidi ya 10. Alitaja maeneo ambayo nyaraka hizo inabidi mwekezaji azitafute na kuwa nazo jambo linaloongeza urasimu na ukiritimba katika uwekezaji nchini kuwa ni Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA), Wakala wa Usajili Biashara na Utoaji Leseni (BRELA), Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Akizungumzia suala la kodi, Bashe alisema serikali inabidi kufikiria kupunguza utitiri huo wa kodi ikiwa ni pamoja na kuzindoa zile zisizo za lazima. “Kwa mfano kuzalisha square feet ya ngozi Tanzania ni senti dola za Marekani senti 14 wakati Ethiopia ni dola za Marekani senti nane na India dola za Marekani senti saba. Tutawezaje kushindana?”

Kwa upande wake, mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto, amesema itakuwa ndoto kwa Tanzania kwenda kwenye uchumi wa viwanda bila kufungamanisha sekta nyingine zikiwemo za kilimo na uzalishaji wa malighafi.

Amesema kwa hali ilivyo inaonyesha wazi kuwa viwanda vingi nchini vimepunguza uzalishaji kutokana na ukweli kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mwaka jana Tanzania iliuza bidha za viwanda zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.4 ambapo pia takwimu za mwaka huu zinaonyesha mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameshuka kwa dola za Marekani milioni 500.

XS
SM
MD
LG