Tangazo hilo limekuja miezi nane baada ya Rais Felix Tshisekedi kushinda uchaguzi wa urais uliokuwa umecheleweshwa kwa muda mrefu.
“Hatimaye serikali imemfikia hili la kuunda serikali,” Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilukamba amesema Jumatatu. “Rais amesaini amri ya kiutendaji na tutanza kazi mara moja.”
Chini ya makubaliano ya serikali ya mseto, nafasi 23 zinakwenda kwa wanachama wa chama cha Tshisekedi cha Direction for Change, wakati nafasi zilizobakia 42 zitajazwa na wanachama wa chama cha Rais mstaafu Joseph Kabila, Common Front for Congo.
Uchaguzi wa Disemba ulikosolewa kwa kuwepo dosari katika vituo vya kupiga kura, ikiwemo kukosekana karatasi za kura na mashine za kupigia kura za kielektroniki kutofanya kazi na kuchelewesha uchaguzi kuendelea hadi nyakati za usiku, na kulazimisha maafisa wa uchaguzi kufanya shughuli zao kwa kutumia tochi.
Kikundi cha wasimamizi wa uchaguzi kilichokuwa kimeandaliwa na Kanisa Katoliki kilisema lilipokea ripoti zisizopungua 544 zikieleza kuharibika kwa mashine za kupigia kura.
Uvunjifu wa amani pia uligubika uchaguzi, ambapo watu wanne waliuawa katika eneo la mashariki ya Kivu Kusini, ikiwa ni pamoja na askari mmoja na afisa wa uchaguzi kuuawa, kutokana na madai ya wizi wa kura.
Uchaguzi kumtafuta mrithi wa Rais aliyekuwa anaachia madaraka Joseph Kabila, ulikuwa hapo mwanzoni umepangwa kufanyika mwaka 2016, lakini ulisitishwa baada ya Kabila kukataa kuachia madaraka mwisho wa muhula wake. Kabila alikuwa ametawala DRC tangu baba yake alipouawa mwaka 2001.
Hapo awali uchaguzi ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 23, lakini uliahirishwa kwa kipindi cha wiki mmoja kwa sababu ya moto uliyotokea katika ghala katika mji mkuu wa Kinshasa mapema mwezi huo na kuteketeza maelfu ya mashine za kupigia kura.
Kadhalika maafisa wa uchaguzi waliamua kuchelewesha uchaguzi kufanyika katika miji mitatu hadi mwezi Machi. Miji iliyoko mashariki ya Beni na Butembo yalikumbwa na maradhi ya Ebola. Mji uliyoko magharibi wa Yumbi ulikumbwa na ghasia za kikabila. Kitendo cha kuchelewesha upigaji kura katika maeneo hayo matatu liliwaathiri zaidi ya wapiga kura milioni moja.