Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 13:44

Tshisekedi athibitishwa kuwa rais mteule wa DRC


Felix Tshisekedi
Felix Tshisekedi

Mahakama ya Katiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jumamosi imemuidhinisha rasmi Felix Tshisekedi kama rais aliyechaguliwa kwenye uchaguzi wa Desemba 30 mwaka jana.

Katika uamuzi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na raia wa nchi hiyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali shauri la mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu, ambaye alikuwa anadai kwamba matokeo ya awali yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini DRC, CENI, hayakuwa halali.

Katika uamuzi wao, majaji wa mahakama hiyo walisema kuwa Fayulu hakutoa ushahidi wa kustosha kuonyesha kwamba kura zake zilikuwa zimeibwa.

Kufuatia uamuzi wa mahakama hiyo, ambayo ndiyo yenye kauli ya mwisho kuhusu masuala ya uchaguzi, sasa Tshisekedi anaweza kuapishwa wakati wowote.

Takwimu zilizo tangazwa na CENI katika matokeo yake ya awali zilimwonyesha Tshisekedi akiwa amepata kura milioni 7, sawa na asilimia 38 ya kura zote zilizopigwa.

Alifuatiwa na Martin Fayulu aliyeungwa mkono na watu milioni 6.3, huku Emmanuel Ramazani Shadary wa muungano wa vyama tawala - na ambaye alikuwa anungwa mkono na rais wa sasa, Jeseph Kabila, akiwa katika nafasi ya 3 kwa kuzoa kura milioni 4.3.

Wagombea wengine - ambao walikuwa takriban ishirini - waliambulia kura kiduchu.

Martin Fayulu
Martin Fayulu

Tangazo hilo la CENI lilizua utata na kupingwa na baadhi ya wadau, wakiwemo waangalizi wa kimataifa na kanisa Katoliki, huku baadhi walitaka kura hizo zihesabiwe upya.

Aidha Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya maendeleo ya Afrika kusini (SADC) ni kati ya taasisi zilizo kuwa na misimamo iliyokinzana kuhusu jinsi ya kutatua mzozo ulioibuliwa na tangazo la CENI.

XS
SM
MD
LG