Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 18:27

Uchaguzi wa Kihistoria DRC 2018


Mamia ya waandamanaji mjini Beni, DRC wakipinga kuahirishwa uchaguzi kutokana na ugonjwa wa Ebola, Disemba 27, 2018.
Mamia ya waandamanaji mjini Beni, DRC wakipinga kuahirishwa uchaguzi kutokana na ugonjwa wa Ebola, Disemba 27, 2018.

Wapiga kura nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili wanashiriki katika uchaguzi wa kihistoria ambao kwa mara ya kwanza tangu uhuru, watamchagua rais atakaye kabidhiwa madaraka kutoka kwa mtangulizi wake aliyekuwa amechaguliwa kidemokrasia.

Uchaguzi huo umeahirishwa mara kadhaa tangu muda wa muhula wa Rais Joseph Kabila kumalizika miaka miwili iliyopita na hakuna aliyekuwa na uhakika utafanyika hadi kiongozi huyo alipotangaza mwezi Agosti kwamba hatagombania tena katika uchaguzi wa rais ujao.

Katika makala haya maalum Mwandishi wetu Abdushakur Aboud anatupia jicho changamoto zilizo sababisha kuahirishwa uchaguzi huo na umuhimu wake katika utaratibu wa Demokrasia ya Congo.

Uchaguzi wa DRC
please wait
Embed

No media source currently available

0:00 0:05:05 0:00

Historia ya uchaguzi wa DRC

Tangu kujinyakulia uhuru kutoka ubelgiji Juni 30, 1960, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haijapata kuwa na kipindi kirefu cha utulivu au kuweza kukabidhiana madaraka kwa amani kutoka utawala mmoja hadi mwengine kupitia mfumo wa kidemokrasia

Hivyo uchaguzi huu wa nne tangu uhuru ni muhimu kwani matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliofanyika Julai 30, 2006, yalisababisha mapigano makali katika mji mkuu wa Kinshasa kati ya wafuasi wa Kabila na mpinzani wake mkuu Jean Pierre Bemba.

Kabla ya duru ya pili

Kabla ya duru ya pili Rais Kabila alikutana na wapinzani wake kwa mara ya kwanza baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.

Jean Pierre Bemba alitoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuhakikisha usalama katika uchaguzi huo.

“Ninatowa wito kwa jumuia ya kimataifa kuchukua wajibu wa kuhakikisha usalama wa mji huu, usalama wa nchi hii. Kwani hiyo ndio sababu ya wao kuwepo hapa.”

Uchaguzi ulifanyika Oktoba na Kabila kutangazwa mshindi lakini kulizuka ghasia mpya mashariki mwa nchi hiyo; likihusisha kwanza ni kundi la Laurent Nkunda CNDP, ikifuatwa na kundi la M23 la Bosco Ntaganda.

Baada ya kumalizika kwa muhula wa kwanza wa Rais Kabila, uchaguzi mwengine ukaitishwa hapo 2011 na kukabiliwa na ghasia kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kulikuwepo na wagombea 11 katika uchaguzi huo na Kabila kutangazwa mshindi licha ya malalamiko ya wizi wa kura.

Muhula wa pili na wa mwisho wa Rais Kabila

Muhula wake wa pili na wa mwisho ulipo karibia hapo Septemba 29, 2016, tume huru ya uchaguzi ikatangaza uchaguzi umeahirishwa hadi 2018, kwa vile muda wa kuwaandikisha wapiga kura ulikuwa hautoshi. Jambo hilo lilizusha maandamano na ghasia hadi kanisa Katoliki kuingilia kati na kufikia makubaliano maalum ya Disemba 31, na kumruhusu Kabila kubaki madarakani hadi mwishoni mwa 2017.

Kufikia Julai 7 Rais wa CENI, Corneille Nangaa, alisema uchaguzi hauwezi kufanyika na kusababisha malalamiko mengine hadi ilipotangazwa utafanyika Disemba 23, 2018.

Lakini Wasi wasi uliendelea kuwepo iwapo Kabila atagombania tena au la. Mapema mwezi Agosti alitangaza kwamba hatogombania na hapo ndipo harakati za kweli za kuchukua nafasi yake na baada ya ushauriano wa muungano unaotawala wa FCC, Kabila alimtangaza waziri wake wa mambo ya ndani Emanuel Ramzani Shadari kuchukua nafasi yake.

Na hapo ndipo upinzani ukaamini kuna mashindano makali na katika dakika za mwisho kujaribu kumtafuta mgombea moja wa upinzani.

Upinzani walipo kutana Geneva

Walikutana Geneva na viongozi 7 wa upinzani walimchagua mfanyabiashara Martin Fayulu anaefahamika zaidi Kinshasa kuliko sehemu nyingine za nchi siku mbili baadae makubaliano yalivunjika na Felix Tshisekedi na Vilate Kamere wakajiondoa na kuunda mungano wao.

Hivyo basi kuna wagombea watatu wakuu kati ya 21 wanaogombea kiti cha urais Disemba 30, 2018.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na chuo kikuu cha New York unaonyesha upinzani unaungwa mkono kwa asilimia 70 na Wakongo na asilimia 36 wanamuunga mkono Tshisekedi akifuatiwa na mshirika wake mpya Kameher mwenye asilimia 17 na Shadary nafasi ya tatu asilimia `16 na Fayulu anaungwa mkono kwa asilimia 8.

Macho ya dunia nzima yataelekea Congo kuanzia hivi sasa ambako mvutano ungali unaendelea juu ya kompyuta za upigaji kura, ambapo CENI inadai ndio njia pekee ya kuepusha wizi wakati upinzani ukidai si watu wote wanaweza kutumia mashine hiyo. Cha muhimu wakongo wanatarajia uchaguzi kuwa haki, huru na wa amani.

XS
SM
MD
LG