“Wakati habari za kuachiwa kwa Kabendera zimepokelewa kwa furaha baada ya kukaa jela karibuni miezi saba, inashitusha kuona kuwa amelazimishwa kulipa kiwango kikubwa cha faini ili kupata uhuru wake, baada ya kuwa aliwekwa mahabusu kwa uonevu kwa sababu alikuwa anatumia haki yake ya uhuru wa kujieleza.
“Mama yake Kabendera alikufa wakati yeye yuko mahabusu kipindi kifupi baada ya kutoa maombi yake kwa Rais John Magufuli kupitia kituo cha televisheni kwamba amwachie huru mtoto wake.
Taarifa ya Amnesty International inasema kuwa tayari Kabendera ameteseka kwa kiasi kikubwa kwa kutekeleza wajibu wake wa Kiuandishi na alistahili kuachiwa bila masharti yoyote.
"Hakuna haki kabisa katika kile kilichofikiwa mahakamani mjini Dar es Salaam hivi leo," amesema mkurugenzi huyo.
Ameongeza : “Tanzania lazima iache kutumia vibaya sheria zinazotumika kukiuka haki za watu katika kutumia uhuru wao, uhuru wa kujelezea na kupashwa habari, kukusanyika kwa amani na kujiunga na chama wanachotaka."
Shirika hilo limesisitiza kuwa :"Ni lazima nchi ichukue ahadi hadharani kwamba itamhakikishia kila mtu ana uhuru wa kutumia haki zao zote za kibinadamu na kuacha kutumia sababu zinazochochewa na siasa kuwabana wapinzani na waandishi kama Eric Kabendera.”
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.