Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Januari 25, 2025 Local time: 03:21

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aanza ziara ya siku nane Mashariki ya Kati na Asia


Blinken
Blinken

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ameanza ziara ya siku nane huko Mashariki ya Kati na Asia.

Ziara ya Blinken inaanzia Israel wakati ambapo nchi hiyo imeongeza mashambulizi ya kulipiza kisasa dhidi ya kundi la Hamas huko Gaza.

Kabla ya kuondoka Washington, waziri Blinken alifanya mazungumzo na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika AU.

Antony Blinken, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani amesema: "Uhusiano kati ya Marekani na Umoja wa Afrika ni mfano bora wa nia yetu na imani yetu kwamba linapokuja suala la Afrika, sio kile tunachofanya kwa Afrika, ni kile tunachofanya na Afrika na kuiunga mkono Afrika."

Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, awamu ya kwanza ya safari yake inaanza na mkutano mwingine na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na viongozi wengine wa Serikali ya Israel ili kupata taarifa kuhusu malengo ya wanajeshi wao.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Msemaji huyo aidha aliongeza kuwa Blinken atafanya mazungumzo na Israel kujadili umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kupunguza vifo vya raia.

Wizara ya Mambo ya Nje ilisema, Blinken akiwa Jordan atasisitiza dhamira ya pamoja kati ya Marekani na Jordan ili kuwezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu kuwafikia raia wa Gaza.

Mfalme wa Jordan Abdullah II
Mfalme wa Jordan Abdullah II

Mapema Jumatano, Jordan ilitangaza kumrudisha Balozi wake kutoka Israel kupinga mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, ikielezea jinsi watu wasio na hatia walivyofariki na kusababisha mgogoro wa kibinadamu.

Jordan ilisema kuwa Balozi wake atarejea Tel Aviv iwapo Israel itasitisha harakati zake za kijeshi huko Ukanda wa Gaza.

Hii ni safari ya pili ya Blinken kuelekea Mashariki ya Kati tangu shambulizi la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba. Marekani imekuwa ikitoa msaada kwa vita vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas na kuwezesha misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina huko Gaza.

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, mgogoro unaoendelea Israel na eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu umesababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi ya raia. Huko Ukanda wa Gaza, mashambulizi ya anga na ukosefu wa vifaa vya matibabu, chakula, maji na mafuta vimemaliza mfumo wa afya ambao tayari hauna rasilimali.

Dkt Richard Peeperkorn, Mwakilishi wa WHO: “WHO inataka upatikanaji wa haraka na wa misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na chakula, maji, chakula na vifaa vya matibabu ndani na katika ukanda wa Gaza.”

Hospitali zimekuwa zikifanya kazi zaidi ya uwezo wake kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa pamoja na raia waliokimbia makazi yao wanaotafuta makazi. Utoaji wa huduma muhimu za afya - kutoka kwa mama na mtoto mchanga hadi matibabu ya magonjwa sugu yameathiriwa sana.

Watu wakisubiri katika kivuko cha mpakani eneo la Rafah linalopakana na Misri kusini mwa Ukanda wa Gaza, November 1, 2023.
Watu wakisubiri katika kivuko cha mpakani eneo la Rafah linalopakana na Misri kusini mwa Ukanda wa Gaza, November 1, 2023.

Wakati huohuo Mamia ya wasafiri wa kigeni wakiwa na passpoti zao walionekana wakiwasili siku ya Alhamisi kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Gaza na Misri.

Magari ya wagonjwa pia yalikuwa tayari kwenye kivuko hicho kuwapokea Wapalestina waliojeruhiwa.

Kufunguliwa kwa kivuko cha mpaka cha Rafah siku ya Jumatano, kuruhusu mamia ya wenye hati za kusafiria za kigeni na Wapalestina waliojeruhiwa kuondoka Gaza, kulifuatia mazungumzo ya wiki kadhaa kati ya Misri, Israel, Marekani na Qatar, ambayo ni mpatanishi na Hamas.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Hubbah Abdi, Washington.

Forum

XS
SM
MD
LG