Netanyahu alikua akizungumza wakati jeshi la nchi kavu la nchi yake lilikua linapambana na wapiganaji wa Hamas ndani ya Gaza, huku jeshi la anga likidondosha mabomu kwenye ukanda huo.
Kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel, balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu aliitisha Jumatatu mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili hali huko Gaza.
Afrika Kusini nayo, imeutaka Umoja wa Mataifa kupeleka kikosi cha dharura kuwalinda raia wa Palestina huko Gaza baada ya Israel kuongeza mashambulizi yake.
Kwa miaka yote Afrika ya Kusini imekua ikitoa wito wa kupatikana amani katika kanda ya Mashariki ya Kati na ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa vita vya Wapalestina tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru wake 1994.
Kwenye kikao cha Jumatatu cha Baraza la Usalama, mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Palestina, Philippe Lazzarini, amesema wakazi wa Gaza wanakumbwa na adhabu ya pamoja na kulazimishwa kuhama, wakati Israel inadai inawatafuta wapiganaji wa Hamas.
Amesema usitishaji mapigano kwa ajili ya huduma za binadamu umekua suala la uhai na mauti kwa mamilioni ya watu.
Amesema kuwaadhibu watu kwa pamoja na kuwalazimisha watu kuhama ni mambo yanayoweza kufikia kiwango cha uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa vita.
Wakati huo huo Marekani inasema inafanya kila juhudi kuongeza msaada wa dharura huko Gaza wakati Umoja wa Mataifa ukionya kwamba idadi ya malori yanayoruhusiwa kuingia ni kidogo sana kuweza kukidhi mahitaji ya wapalestina.
Ni malori 33 yaliyoruhusiwa kuingia siku ya Jumapili.
Forum