Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:29

Tundu Lissu atangaza nia ya kuwania urais Tanzania


Tundu Lissu
Tundu Lissu

Aliyekuwa mbunge wa Singida mashariki na mwanasiasa maarufu wa upinzani, Tundu Lissu, ametangaza rasmi nia ya kugombea urais nchini Tanzania katika uchaguzi wa Oktoba, 2020.

Lissu ametangaza nia ya kugombea urais akiwa nje ya nchi.

Katika hotuba yake ya dakika 37 sekunde 42 kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, Lissu, wakili ametangaza kuwasilisha maombi ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake cha Chadema.

Lissu, mwenye umri wa miaka 52 ambaye yupo uhamishoni tangu aliposafiri nje ya Tanzania kwa matibabu baada ya kunusurika kifo alipopigwa risasi 16 na watu ambao hadi sasa hawajulikani, ameangazia ukandamizaji, demokrasia na haki za binadamu katika maelezo yake aliyoyatoa wakati wa kutangaza nia ya kuwania nafasi ya juu ya uongozi nchini Tanzania.

Madai ya Lissu kuhusu utawala wa Magufuli

Lissu amedai kwamba utawala wa miaka mitano wa Rais wa sasa John Pombe Magufuli, unaomalizika mwaka huu, umeiweka Tanzania katika mtihani mkubwa kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia. Amesema Tanzania ipo katika njia panda na uchaguzi mkuu wa Oktoba ni muhimu sana katika kurejesha uhai wa nchi.

“Badala ya kuzingatia mazingira halisi ya kiuchumi ndani na nje ya nchi yetu, Rais Magufuli ameendesha uchumi wetu bila sera au mipango madhubuthi ya kiuchumi bali kwa kutumia amri za kiutendaji na majukwaa ya siasa.

Bila sera inayoeleweka au mipango thabithi ya kiuchumi au ya kibiashara, sasa serikali yetu imejiingiza kwenye biashara kuanzia kuuza na kununua mazao ya biashara, mabenki, uchimbaji madini, hadi biashara ya kuendesha shirika la ndege” amesema Tundu Lissu.

Lissu ameongeza kwamba “Kwa kutumia njia hizo za amri za kisiasa, vyombo vya ulinzi na usalama vikiwemo jeshi la wananchi la Tanzania, jeshi la polisi, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, na idara ya usalama wa taifa pamoja na mamlaka ya kodi TRA, vinatumika kukamata kwa nguvu na kutaifisha mali za wafanyabiashara wetu wa ndani na makampuni ya wawekezaji kutoka nje. Hata wakulima wadogo wa vijijini hawajaachwa salama kama ilivyotokea kwenye zao la korosho mwaka jana ambapo wakulima walinyang’anywa zao lao kwa nguvu za kijeshi na ukatili mkubwa kwa amri ya rais Magufuli mwenyewe”.

Kulingana na Lissu, miaka mitano zaidi ya Magufuli itakuwa ya kuharibu zaidi uchumi wa Tanzania, mfumo wa demokrasia, haki za binadamu na maslahi ya jumla ya nchi.

Haki za kibinadamu Tanzania

Lissu amedai kwamba haki za kibinadamu na utawala wa sheria umechanwa vipande vipande na Tanzania imekuwa nchi ya vilio na machozi, utekaji nyara,mateso na ukandamizaji kwa wakosoaji wa serikali kwa kuwafungulia kesi za kupandikiza, mauaji ya wananchi, ukosefu wa uhuru wa vyombo vya habari ni baadhi ya mambo Lissu amemkosoa Magufuli wakati anatangaza nia yake ya kugombea urais, akitoa orodha ya watu wanaodaiwa kupotea, kuuawa, kukamatwa au kuteswa wakati wa utawala wa Magufuli. Orodha hiyo ni Pamoja na wanasiasa, wafanyabiashara na waandishi wa habari.

“Nchi yetu imekuwa nchi ya wajane, yatima na vilema” amedai Lissu na kusema kwamba “ndani ya miaka 5 ya utawala huu, utaratibu wote wa haki za biandamu na utawala wa sheria umechanwa vipande vipande na serikali ya rais Magufuli na vyombo vyake vya ulinzi na usalama”.

Amewasilisha taarifa rasmi ya kutangaza nia ya kugombea urais kwa katibu mkuu wa chama cha Chadema, miongoni mwa vigezo vyake na sifa za kuwania urais ikiwa ni pamoja na kupigania katiba mpya, kuwa rais wa chama cha mawakili kabla ya uongozi wake kukatizwa kikatili kwa kupigwa risasi 16, kuwa na msimamo thabithi katika kutetea maslahi ya raia na taifa kwa jumla, akidai kuboresha uchumi, demokrasia, kushughulikia kile amekitaja kama kilio na hofu ya watanzania, na kuwaondoa katika kile alichodai maisha ya ukandamizaji.

Tundu Lissu amesisitiza kwamba hana doa lolote maishani mwake, hajawahi kushitakiwa, kutuhumiwa, au kuadhibiwa mahakamani na kwamba hakuna lolote linaloweza kumfutia sifa ya kugombea urais Tanzania, licha ya spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai kumuondoa katika wadhifa wake wa ubunge.

Msimamo wa kisheria kuhusu Lissu

Lakini je,changamoto gani inamsubiri Lissu katika safari yake ya kugombea urais Tanzania, ikizingatiwa kwamba ametangaza nia akiwa nje ya nchi? James Masawe ni mwanasheria, Tanzania.

“Ajenge hoja kabla ya chama chake kumteua. Auze hoja zake kwa wananchi kama anaamini wananchi wanaweza kumteua kuwa rais. Kwa hivyo sidhani kama kuna hoja yeyote kisheria kumzuia Tundu lissu kugombea urais Tanzania”, amesema mwanasheria Masawe.

Tundu Lissu ameahidi hatolipiza kisasi kwa kupigwa risasi na badala yake kuongoza maridhiano, linajadiliwa sana kwenye mitandao ya kijamii nchini humo kwa hisia tofauti, wafuasi wa chama tawala CCM wakimkosoa vikali huku upande wa upinzani wakikaribisha hatua hiyo.

Uchaguzi wa Tanzania utafanyika tarehe 25 Oktoba mwaka huu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG