Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 15:55

Tigray kwenye hatari ya njaa, USAID yasema


Mkuu wa USAID, Samantha Power
Mkuu wa USAID, Samantha Power

 Marekani imeonya kwamba huenda msaada wa chakula utamalizika wiki hii kwa mamilioni ya wakazi wa eneo lililokumbwa na mzozo kaskazini mwa Ethiopia, la Tigray.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, mkuu wa shirika la marekani kwa ajili ya maendeleo ya kimataifa,USAID, Samantha Power, kupitia taarifa mwishoni mwa wiki alisema kwamba ni chini ya asilimia 7 ya chakula kinacho hitajika, ambacho kinafika Tigray.

Eneo hilo linasemekana kuwa na wakazi takriban milioni 6 wakati USAID pamoja na mashirika mengine ya kutoa misaada yakisemekana kumaliza chakula kwenye ghala zao kutokana na miezi 9 ya mapigano.

Power ameongeza kusema kuwa uhaba huo sio kwa sababu ya ukosefu wa chakula, mbali ni kutokana na serikali ya Ethiopia kuzuia upelekaji wa misaada kwenye eneo hilo.

USAID linasema kwamba tayari watu 900,000 kwenye eneo la Tigray wanakabiliwa na hali ya njaa, ikisemekana kuwa ni janga baya zaidi la kibinadamu katika kipindi cha muongo mmoja. Shirika la habari la AP linasema kuwa tayari kuna watu waliokufa kutokana na njaa.

Serikali ya Ethiopia kwa upande wake inadai kuwa mashirika ya kutoa misaada yanapeleka silaha pamoja na kushirikiana na vikosi vya Tigray. Baadhi ya wafanyakazi wa kutoa misaada wanadai kwamba upekuzi umekuwa ukifanywa kwenye vifaa na bidhaa zao wakati wakijaribu kupeleka misaada kwenye eneo hilo.

Msemaji wa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Billene Seyoum amekanusha madai ya Power. Matamshi ya Power yalikuja muda mfupi baada ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuwaambia wanahabari kwamba hali huko Tigray ni kama jehanamu.

XS
SM
MD
LG