Lalibela pia ni eneo takatifu kwa mamilioni ya wakristo wa ki Orthodox kwenye eneo la Wollo lililoko kwenye jimbo la Amhara kaskazini mwa Ethiopia. Katika wiki za karibuni , mapigano yameenea kutoka Tigray hadi kwenye majimbo ya Amhara na Afar, wakati yakisababisha takriban watu 250,000 kutoroka makwao.
Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Marekani waliotembelea eneo hilo wiki hii, wamesema kuwa kuna wasi wasi wa kuenea kwa mapigano kwenye maeneo mengine kaskazini mwa Ethiopia. Marekani Alhamsi imeomba vikosi vya Tigray kuheshimu turathi zilizopo Lalibela wakati ikieleza wasi wasi wa kuongezeka kwa ghasia nchini humo.
Seyfu ambaye ni mkazi wa Lalibela akizungumza na Reuters kwa njia ya simu alisema kuwa aliona mamia ya watu wenye silaha, waliokuwa wakizungumza lugha ya Tigrinya wakati wakitembea kwenye mji huo Alhamisi. Seyfu aliongeza kusema kuwa vikosi kutoka jimboa la Amhara ambao wana uhusiano na serikali kuu, walitoroka Jumatano usiku wakiandamana na maafisa wa mji huo.
Imetayarishwa na Harrison Kamau