Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 15:30

Vikosi vya Oromo vyadai kufanya mkataba na TPLF, Ethiopia


Wanajeshi kutoka kundi la Oromo, OLA ,katika picha ya maktaba
Wanajeshi kutoka kundi la Oromo, OLA ,katika picha ya maktaba

Kiongozi mmoja wa kundi lenye silaha nchini Ethiopia Jumatano amesema kuwa kundi lake limefanya makubalino na vikosi vya Tigray kwa nia ya kuelekea kwenye mji mkuu wa taifa hilo, wakati ghasia zilizoanzia Tigray mwaka uliyopita zikionekana kuenea kwenye maeneo mengine ya taifa hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, kiongozi wa kundi la Oromo Liberation Army, OLA, Kumsa Diriba ambaye pia anajulikana kama Jaal Marroo amesema kuwa suluhisho kwa sasa kwenye taifa hilo la pili lenye watu wengi barani Afrika, ni kuzungumza lugha ambayo serikali kuu ilianzisha.

Diriba amesema kuwa mashauriano yake na kundi la TPLF yalianza wiki kadhaa zilizopita, baada ya Tigary kutoa pendekezo hilo. Ameongeza kusema kwamba wamekubaliana kushirikiana dhidi ya adui mmoja. Diriba pia amesema kuwa makundi mengine yenye silaha nchini humo yanaendelea kushauriana kwa lengo la kuunda muungano mmoja dhidi ya serikali ya Abiy.

Msemaji wa TPLF Getachew Reda, wiki iliyopita aliambia AP kwamba ni kweli walikuwa kwenye mashauriano na watu wengine kwa lengo la kufikia makubaliano fulani ya kisiasa bila kutoa maelezo zaidi. Hata hivyo hakuna tamko lolote lililotolewa kutoka ofisi ya waziri mkuu.

Tangazo la kiongozi wa OLA, limekuja siku moja baada ya waziri mkuu kutoa wito kwa wale ambao wangetaka kujiunga na jeshi la serikali, ili kuangamiza TPLF. Taarifa hizo ni uthibitisho wa kuenea kwa ghasia za Tigray zilizoanza Novemba mwaka jana baada ya mzozo wa kisiasa kati ya waziri mkuu Abiy Ahmed na viongozi wa Tigray ambao kwa karibu miongo mitatu walikuwa kwenye utawala wa taifa hilo.

Tangu wakati huo maelfu ya watu wameuwawa kwenye mapigano hayo wakati kukiwa na madai ubakaji, njaa na ukatili mwingine kutoka kwa watu wa kabila la Tigrinya.

Mtayarishi- Harrison Kamau

XS
SM
MD
LG