Shirika la ndege la Ethiopia limekanusha madai kwamba limekuwa likisafirisha silaha na wanajeshi kwenda katika eneo lenye vita katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Tigray.
Hayo yamejiri kufuatia wito uliotolewa kwa abiria kulisusia shirika hilo la ndege lililo kubwa zaidi la kubeba abiria barani Afrika linalomilikiwa na serikali ya Ethiopia lilioonekana kwenye mitandao ya kijamii likishutumiwa kuhusika katika mzozo huo miezi tisa kati ya serikali na wapiganaji wa chama cha TPLF cha Tigray.
Madai ya kuhusika kwa shirika hilo yalichapishwa katika kurasa za mtandao wa Twitter mengine yakiandamana na picha za wanajeshi waliopanda moja ya ndege zake.
Shirika hilo hata hivyo limesema madai hayo hayana msingi wowote. Shirika hilo limesema ripoti hizo "zilitumia picha kadhaa za zamani na zisizohusiana kwa njia yoyote, kwa nia ya kuliharibia jina".
Safari za Ndege za kwenda na kurudi kutoka katika jimbo la Tigray zilisitishwa baada ya mzozo kuzuka mwezi Novemba mwaka 2020.
Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yametoa wito wa dharura wa kufunguliwa kwa njia za angani na za ardhini kwenda Tigray, ambapo yanaeleza kwamba zaidi ya watu milioni tano wanahitaji msaada.