Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 20:48

Tanzania yaombwa iweke mfumo wa elimu kumlinda mwanafunzi wa kike dhidi ya rushwa ya ngono.


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Picha na HANNAH MCKAY / POOL / AFP
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Picha na HANNAH MCKAY / POOL / AFP

Mabadiliko ya mfumo wa elimu yanaweza kuchangia kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa rushwa ya ngono ambayo husababisha matatizo kwa wasichana na kuathiri maendeleo na haki zao hususani wale walio katika vyuo vya elimu ya juu.

Wakati maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike ambayo hufanyika Oktoba 11 kila mwaka, baadhi ya wanafunzi wakike wanaosoma katika vyuo vikuu nchini Tanzania walitoa wito kwa serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa elimu ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya rushwa ya ngono.

Aidha wanafunzi hao wamesema mfumo uliopo unaonekana kutoa mianya ya rushwa kwa walimu wa wasichana hao, na kusistiza sheria zilizopo huwalinda walimu hao mara inapogundulika kuna suala la rushwa limetokea.

Happyness Mkomimikinda rais wa serikali ya wanafunzi chuo cha Bahari (DMI) kilichopo jijini Dar es Salaam amesema mfumo uliopo unampa mwalimu uwezo wa kumbana mwanafunzi pale anaposhindwa kufaulu masomo yake na hivyo kumtaka atoe mwili wake ili aweze kusaidiwa.

“Unakuta mwanafunzi hajafaulu vizuri katika masomo yake, kwahiyo mwalimu ana uwezo wa kumbana mwanafunzi ili aweze kumsaidia kwa kitu chochote,” alisema Mkomimikinda na kuongezea “unakuta mwanafunzi hayupo huru kufanya mambo mengine anajikuta anaingia katika hali ya kuutoa mwili wake ili aweze kusaidiwa.”

Waathirika wa vitendo hivyo wanapopeleka malalamiko yao katika ngazi za juu, sheria hazifuatwi na huwalinda waathirika hao.

Bunge la Tanzania huko Dodoma Machi 30, 2021. Picha na AFP.
Bunge la Tanzania huko Dodoma Machi 30, 2021. Picha na AFP.

Makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi katika Chuo Cha Uhasibu Arusha, Tedy Mbaga amesema serikali inapaswa kusimamia sheria zilizowekwa dhidi ya wanaoomba rushwa ya ngono pamoja na kuwaelimisha watoto wa kike kuhusu hatua wanazopaswa kuchukua punde wanapokabiliwa na vitendo hivyo.

“Ukimwambia mtu kwamba ukifanya kitu hiki na kukiwepo na ushahidi utafukuzwa kazi, sidhani kama kuna mtu mzima yeyote ambaye anaweza kujiweka kwenye sehemu itakayomsababishia yeye afukuzwe kazi kwasababu ya vitu kama hivi” alisema Makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi katika Chuo Cha Uhasibu Arusha, “Kwahiyo nafikiri ni vyema, watu wasimamie sheria ili mtoto wa kike apewe elimu, wapi apeleke sauti yake iweze kusikika na kufanyiwa kazi.” Aliongeza.

Hata hivyo Makamu wa Rais wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji kilichopo Dar es Salaam Dolice Alchard aliiambia Sauti ya Amerika kuwa serikali inapaswa kuangalia uhuru waliowapa wanachuo kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakiutumia vibaya kwa kuvaa mavazi yasiyo na maadilili hali inayosababisha ongezeko la rushwa ya ngono.

Amesema “mimi nilikuwa nahisi serikali pia itilie mkazo mavazi hata wanachuo wanapoingia chuoni kwasababu unakuta mtu anavaa nusu uchi na anaingia darasani anakaa anajiachia kwasababu hakuna katazo la mavazi hakuna sheria yoyote inayombana yaani ni mtu mzima tu amepewa uhuru kwahiyo ule uhuru unaotolewa sio kwamba kila mtu anaweza kuutumia, wengi wanautumia ndivyo sivyo kwahiyo kuna haja sana ya serikali kupaza sauti.”

Naye Esther Mongi Meneja shirika la World Vision Tanzania, ametoa wito kwa jamii, kumpatia mtoto wa kike elimu na kutatua changamoto zinazowakabili katika kutafuta elimu ni kuisaidia jamii kwa kuwa mtoto wa kike ndio mlezi wa familia na muandaaji wa kizazi kijacho amemalizia kusema.

Imatayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG