Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 21:06

Mpango wa usajili wa bima ya afya kwa watoto wazua mjadala Tanzania


Wanawake wakiwa na watoto wao katika Kituo cha Afya cha kilichopo Sinza, Dar es Salaam Mei 2, 2011. Picha na REUTERS/Emmanuel Kwitema.
Wanawake wakiwa na watoto wao katika Kituo cha Afya cha kilichopo Sinza, Dar es Salaam Mei 2, 2011. Picha na REUTERS/Emmanuel Kwitema.

Mpango wa kubadilisha mfumo wa usajili kwa watoto chini ya umri wa miaka 18 kupata bima ya afya (NHIF) watakapoanza masomo umeibua mjadala na maoni mseto nchini Tanzania.

Mpango huo ambao unapingwa na baadhi ya Watanzania, unakuja baada ya kuibuka sintofahamu ya kuondoshwa bima ya toto afya ambayo hutumiwa na watoto chini ya umri wa miaka 18.

Hata hivyo wizara ya afya imewatoa wasiwasi wananchi na kusema bima hiyo bado inapatikana isipokuwa utaratibu wake ndio umebadilishwa kwa kuanza kusajili watoto walio shule ili kuongeza idadi ya wachangiaji.

Meneja uhusiano wa mfuko wa taifa wa bima ya afya, Angel Mzirahi ameeleza “utaratibu tu ndio umebadilika lakini usajili wa watoto bado unaendelea mtoto alie chini ya miaka 18 wanasajiliwa kupitia shule zao”

Na kuongeza kuwa “lakini pia wale ambao hawasajiliwi kupitia shule upo mlango mwengine ambao wazazi wanaweza wakaingia pamoja na watoto wao.”

Hata hivyo Mzirahi amesisitiza kuwa matibabu yanaweza kuwa ya gharama kubwa, hivyo kuwa na bima ya afya inatoa uhakika na kinga kwa familia dhidi ya mzigo mkubwa wa kifedha unaoweza kutokea kutokana na magonjwa au matatizo ya kiafya.

Aidha, hofu ya wanasiasa na wanaharakati ni kuhusu athari za mabadiliko hayo kwa Watanzania wanaoishi vijijini kwa vile mara nyingi huwa ni waathirika wa kwanza wa mabadiliko yoyote yanapotokea, hali ambayo inasababishwa na mazingira yao ya kiuchumi na upatikanaji mdogo wa huduma za kijamii.

Namoro Saituti (katikati) akiwa na watoto wake katika kijiji cha Msomera Handeni, Tanzania Julai 15, 2022. Picha na AFP.
Namoro Saituti (katikati) akiwa na watoto wake katika kijiji cha Msomera Handeni, Tanzania Julai 15, 2022. Picha na AFP.

Mwalimu Saimoni Lupogo ambaye ni mwakilishi wa wakuu wa shule ngazi ya taifa kanda ya Dar es Salaam amesema ili suala hilo liweze kufanikiwa serikali ibuni mikakati ya kutoa elimu, pamoja na wazazi kuungana.

“kwahiyo mimi ninacho ona hapa suala la msingi ni kuhakikisha tu elimu hiyo inatolewa mapema, wenyeviti wa vijiji, wa vitongoji waitishe mikutano wawaelimishe wazazi namna ambayo wanapaswa kufanya na jambo hilo litakuwa rahisi lakini kama elimu haitatolewa ndipo kutakuwa na uzito katika kutekeleza sera hiyo ya afya.” Alisema Lupogo.

Hata hivyo Naibu Waziri Afya kivuli ACT Wazalendo Ruqayya Nassir amesema afya za Watanzania zimefanywa kuwa chanzo cha mapato kwa serikali na kueneza matabaka kwa wananchi. Huku akiitaka serikali kukaa chini na kufikiria namna bora ambayo itawawezesha Watanzania kugharamia matibabu.

“Kwahiyo bado wanapaswa kukaa chini wafikirie namna bora ya kuwafanya Watanzania kugharamia gharama za huduma ya afya. Alieleza waziri huyo kivuli.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani VOA Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG