Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 15:12

Mataifa zaidi ya 70 yashiriki mkutano mkuu wa mifumo ya chakula Afrika


Viongozi mbalimbali walioshiriki mkutano wa mifumo ya chakula ya Afrika
Viongozi mbalimbali walioshiriki mkutano wa mifumo ya chakula ya Afrika

Maelfu ya washiriki  kutoka mataifa zaidi ya 70 wanakutana katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam nchini Tanzania, kwa ajili ya mkutano mkuu wa Mifumo ya Chakula Afrika.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wamewataka viongozi wa kiafrika kutatua changamoto za masoko baina ya nchi barani humo kwa kuweka sera wezeshi zitakazo mnufaisha mkulima na mfanyabiashara wa mazao ya kilimo.

Wito pia umetolewa kwa nchi za Afrika kuhakikisha kuna upatikanaji wa chakula cha kutosha na kuendeleza biashara huru ili kuboresha usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi katika bara hilo.

Mkutano wa Mifumo ya Chakula ya Afrika
Mkutano wa Mifumo ya Chakula ya Afrika

Mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, Nasoro Kitunda amesema kukosekana kwa mwelekeo wa pamoja wa sera na sheria katika masuala ya biashara ni changamoto kwa nchi za Afrika hali ambayo inaweza kuzuia maendeleo ya biashara baina ya mataifa hayo.

Kitunda anasema hakuna mwelekeo wa pamoja wa sera na sheria katika masuala ya biashara katika nchi nyingi barani Afrika na hali hiyo imekuwa ni changamoto kubwa hasa katika masuala ya ushuru wa forodha na kodi hasa katika mipaka ya nchi mbalimbali.

Wachambuzi wa uchumi wanasema kuna haja ya jitihada za pamoja kati ya mataifa ya Afrika kuunda mfumo wa pamoja wa sera na sheria za biashara, kupitia vyombo vya kikanda ambavyo vitasaidia kusimamia na kuratibu sera za biashara kwa niaba ya nchi wanachama.

Mkurugenzi wa kampuni ya Eat Fresh Tanzania Khadija Jabiri amesema nchi za Afrika zinapaswa kuchukua hatua za kuondoa vikwazo vya kodi na kuanzisha miundombinu ya pamoja ili kuwarahisishia wafanyabiashara kufanya biashara katika bara hilo.

Jabiri anaeleza: “Tuondoe vile vikwazo vya kodi lakini pia kama nchi za Afrika nadhani kuna umuhimu wa kukubaliana kwa pamoja na kuweka miundo mbinu ya pamoja ambayo itarahisisha wafanyabiashara kufanya biashara.

Hata hivyo akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Makamu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango amezitaka nchi za Afrika kupitia mkutano huo kujadiliana kuhusu uwezekano wa kuondoa vikwazo vya biashara kupitia uondoshaji wa kodi zisizo za lazima.

Dkt Mpango alisema: “Ikiwa ni pamoja na kurahisisha mfumo wa usafirishaji wa bidhaa za chakula, kwa hiyo, nazitaka nchi za Afrika kuheshimu mipango ya biashara ya kikanda na hasa mikataba ya biashara huria ya bara la Afrika kwa kuzingatia itifaki za biashara na kuondoa vikwazo vya ushuru.”

Makamu wa Rais amesema serikali za Afrika zinapaswa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapa wakulima wadogo pembejeo za bei nafuu, maarifa, ujuzi na mitaji ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji chakula.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG