Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 15:17

Vijana na wanawake wataka viongozi kubadili mifumo ya uchaguzi, kutoa fursa kwao kukuza demokrasia


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga. Picha kwa Hisani ya LHRC.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga. Picha kwa Hisani ya LHRC.

Vijana na Wanawake wamewataka viongozi nchini Tanzania kubadili mifumo ya uchaguzi wa viongozi ili kuwapa nafasi vijana wa vyama vyote nchini kushiriki katika kukuza na kuendeleza Demokrasia nchini humo badala ya kuegemea katika chama tawala pekee suala ambalo linafifisha Demokrasia.

Hayo yamesemwa hii leo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Demokrasia Duniani ambapo kwa upande wa Tanzania inasherehekea miaka 30 ya demokrasia ya vyama vingi nchini humo.

Akizungumza na Sauti ya Amerika Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Pambalu amesema, ushiriki wa vijana katika upande wa Demokrasia bado upo chini. Huku vijana wakipewa nafasi chache za uongozi na hii inatokana na rushwa miongoni mwa vyama vya siasa hivyo ipo haja ya serikali kuwapa nafasi zaidi vijana.

Pambalu anaelezea "Ushiriki wa vijana katika siasa kwa upande wa Tanzania sio mkubwa sana kwasababu kadhaa rushwa imetawala sana miongoni mwa vyama vya siasa tunaona iko haja ya kuongeza nguvu ya kina katika kuhakikisha kwamba vijana wanashiriki katika Demokrasia wanakuwa ni sehemu ya maamuzi ya kitaasisi ya nchi na maeneo wanayotoka"

Baadhi ya vijana wanaamini kuwa asilimia kubwa ya vijana na wanawake ambao wamekuwa wakipatiwa nafasi za uongozi katika nchi ya Tanzania wanatoka Chama cha Mapinduzi (CCM) hali inayosababisha vijana wengi kukosa chaguo zaidi ya kwenda kujiunga na chama tawala ili waweze kuzifikia ndoto zao.

Deusdedith Soka miongoni mwa wadau wa Demokrasia vijana anasema vijana wengi wamekimbilia kwenye chama tawala kwaajili ya kupata teuzi suala ambalo linawafanya kushindwa kukosoa pale penye mapungufu na kubaki kusifia hali inayofifisha uhuru wa kutoa maoni kwa vijana hao.

Soka anasema "Unakuta vijana wanajua kabisa kwamba ili upate uteuzi kwasababu mamlaka na katiba imempa Rais hiyo nguvu ya kuteua kila mtu ni lazima unakuta vijana wana ile tabia ya kujipendekeza kwahiyo sasa ile Demokrasia ya kumkosoa na ya kukosoa inakuwa haipo kwa vijana."

Hata hivyo Hellen Sisya Naibu katibu Mkuu wa Taasisi ya Young Democrat Union of Africa (YDUA) anasema wanawake wengi ambao wapo katika vyama vya upinzani wamekuwa hawashiriki katika masuala ya Kidemokrasia kutokana na kutopewa nafasi za uongozi na serikali kutokana na wao kuwepo kwenye vyama hivyo.

"Moja ya mambo ambayo yatatusaidia sana kuongeza ushiriki wa wanawake katika michakato ya kidemokrasia ni pamoja na kubadili mifumo yetu tuweze kuwa na tume huru ya uchaguzi ili kila mtu awe na uhuru wa kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi na hivyo tutaongeza pia idadi ya wanawake ambao wanashiriki michakato hii ya kidemokrasia ukiachana na wanawake waliopo kwenye chama tawala peke yao."ameongezea Sisya

Maadhimisho ya siku ya Demokrasia Duniani mwaka 2023 yamebeba kauli mbiu inayosema "kuwezesha kizazi kijacho" ikionesha umuhimu wa kuwapa vijana fursa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kukuza na kuimarisha Demokrasia duniani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),Wakili Anna Henga amemalizia kwa kusema kuwa vijana ndio nguvu kazi ya baadae na wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika mifumo ya kisiasa na kijamii endapo watapatiwa nafasi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Tanzania

Forum

XS
SM
MD
LG