Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 21:50

Mamlaka Tanzania zatakiwa kulinda na kudumisha Amani


Maafisa wa polisi wa kupambana na fujo wakiwa Mji Mkongwe, Zanzibar, Oktoba 29 2020. Picha na MARCO LONGARI / AFP.
Maafisa wa polisi wa kupambana na fujo wakiwa Mji Mkongwe, Zanzibar, Oktoba 29 2020. Picha na MARCO LONGARI / AFP.

Katika maadhimisho ya siku ya Amani duniani, baadhi ya wadau wamewataka viongozi kuhakikisha Tanzania inakuwa mfano bora katika kulinda Amani.

Wakati viongozi wa kisiasa wakisisitiza umuhimu wa kuepuka matumizi ya nguvu dhidi ya raia na kuhakikisha uhuru wa kujieleza na kushiriki katika siasa unaheshimiwa.

Wasomi na viongozi wa dini wamewasihi viongozi waliopo madarakani ambao ni walinzi wakubwa wa Amani, kutumia madaraka waliyopewa kuimarisha na kudumisha amani nchini.

Innocensia John, mchumi kutoka Dar es Salaam amesema watawala wana nafasi kubwa katika kudumisha amani kwa kuhimiza mshikamano baina ya Watanzania.

“Watawala wana kazi kubwa mno katika kudumisha amani, kwasababu ukiongoza watu, mara nyingi kuna tabia ya kuwafuata wale viongozi, kwahiyo wakihimiza mshikamano, amani na upendo basi watu wanao watawala watafuata nyayo zao.” Amesema John.

Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Uchumi na Amani (IEP) ya mwaka 2023. Inaonyesha kwamba Tanzania inashika nafasi ya 17 kati ya nchi za Afrika kwa kuwa na amani. Ripoti hiyo inaonyesha Mauritius ikiongoza kwa amani katika bara la Afrika.

Akizungumza na sauti ya Amerika Askofu wa Dayosisi ya Karagwe Benson Bagonza amesema amani katika bara la Afrika inavunjwa zaidi na waliopo madarakani kuliko na wale wanaotawaliwa, hivyo jukumu la kuilinda amani wanalo zaidi viongozi.

Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema, katika viwanja vya Furahisha huko Mwanza Januari 21, 2023. Picha na Michael JAMSON/AFP
Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema, katika viwanja vya Furahisha huko Mwanza Januari 21, 2023. Picha na Michael JAMSON/AFP

Askofu Bagonza amesema “Mimi ninaona amani inavunjwa na wale walio madarakani kuliko kuvunjwa na wale wanao tawaliwa, kwasababu walio madarakani ndio wana nguvu ndio wana silaha zinazoweza kutumika kuvunja Amani, ndio wana maamuzi yanayoweza kufanyika kibabe.”

Aidha Askofu Bagonza amesisitiza umuhimu wa viongozi walio madarakani katika kulinda Amani na umuhimu wa amani katika kujenga ushirikiano baina ya serikali na wananchi.

Naye Mkuu wa Oganaizesheni na Utawala wa chama cha NCCR Mageuzi Florian Rutayuga amesema serikali inapaswa kutenda haki, kuwasikiliza wananchi na kuacha kutumia nguvu za jeshi la polisi ili kuendelea kulinda amani iliyopo.

“Serikali itende haki, iwasikilize watu isitumie nguvu na hasa kwa kutumia jeshi la polisi.” Amesema Rutayuga.

Na kuongeza kuwa “nimeona kwamba jeshi la polisi limekuwa likitumika pasipo kujua kama linatumika kwasababu hii nchi ni yetu sote kwahiyo, tunatakiwa sisi sote tunufaike na taifa hili.”

Imetayarishwa na Amri Ramadhani sauti ya Amerika Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG