Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 13:01

Rwanda yasema itashirikiana na dunia, huku DRC ikitaka kusimamia amani yake


Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Septemba 20 2023. Picha na Cia Pak / UMOJA WA MATAIFA / AFP
Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Septemba 20 2023. Picha na Cia Pak / UMOJA WA MATAIFA / AFP

Rwanda Jumatano imesema ipo tayari kushiriki kikamilifu kutafuta suluhisho la matatizo ya kidunia, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiutaka Umoja wa Mataifa kushirikiana nayo kikamilifu kuleta amani yake, huku kwa mara nyingine ikiinyooshea kidole Rwanda.

Baada ya mivutano baina ya mataifa ya Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, katika mkutano wa mwaka jana wa 77 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, majirani hao wawili Jumatano walijikita zaidi katika masuala muhimu ya kikanda na kidunia.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi
Rais wa DRC Felix Tshisekedi

Rais wa Rwanda Paul Kagame, yeye aliahidi utayari wa taifa lake katika kushiriki kikamilifu kutatua masala yanayo ukabili ulimwengu kwa sasa.

Alisema, licha ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza Covid-19, si janga tena la dunia, athari zake bado zinaendelea kusumbua mataifa mengi hasa yanayo endelea.

Kutokana na hayo, ameisihi taasisi kubwa za kifedha, kuangalia namna ya kupunguza mzigo unaoyaelemea mataifa masikini. Pia amesisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika kushirikishwa kikamilifu katika masuala ya kidunia.

Kwa upande wa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, ameutaka Umoja wa Mataifa, kushirikiana kwa ukaribu na DRC kutatua mzozo wa mashariki mwa nchi.

Amesema kwa sasa nchi yake ipo tayari kuchukua jukumu la kuleta amani yenyewe, na kuna haja ya kutathimini kazi ya tume ya usimamizi wa amani ya Umoja wa Mataifa, DRC, (MONUSCO) kwa kuwa haionekani kuleta mafanikio.

Amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo kwa wote wanao husika na ufadhili wa kundi la uasi la M23, na kuongeza baraza liwe na usawa wa kushughulikia masuala mengine ya Afrika, kama mzozo wa Sahara Magharibi, mapinduzi ya magharibi mwa Afrika, Sudan na ugaidi unaiokabili Msumbiji.

Alhamisi, rais William Ruto, atahutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa, akiwa na mtaji wa kupongezwa na viongozi mbalimbali akiwemo rais wa Marekani, Joe Biden, kwa kuongoza juhudi za kuleta utulivu katika taifa la Haiti, ambalo linakabiliwa na machafuko kwa sasa.

Tanzania, ambayo inawakilishwa na makamu wake wa rais Phillip Mpango, itawasilisha ujumbe wake na kutoa mwelekeo na msimamo wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Idd Ligongo, New York

Forum

XS
SM
MD
LG