Balozi wa Tanzania nchini Israel Alex Kalua amesema hali inaendelea kuwa ya tahadhari huku watanzania wawili hawajulikani walipo na mwingine mmoja amepatikana baada ya shambulio la Hamas nchini Israel mwishoni mwa juma. Kuna jumla ya watanzania wapatao 260 nchini humo ambao wengi wao ni wanafunzi.
Kwa mujibu wa balozi huyo serikali ya Israel imewataka wasikae kwa wasi wasi na wanaendelea kupata taarifa kutoka kwao kila jioni na wameeleza kuwa ikiwa kuna kundi lolote litahitaji kuondoka nchini humo linaweza kwani viwanja vya ndege vyote vinafanya kazi kama kawaida.
Baadhi ya maeneo ya Tel Aviv na Kusini mwa Israel kulikuwa na taharuki lakini mamlaka za nchi hiyo zinatoa taarifa kwa umma na kila nyumba ina eneo salama la kujificha (Shelter) na iwapo ikitokea tahadhari watu wanaweza kukimbulia maeneo hayo salama.
Mamlaka imewatahadharisha wananchi kutotoka nje na wakae karibu na nyumba zao ili ikitokea hatari wapate fursa ya kukimbilia kwenye eneo salama kwa urahisi.
Forum