Wakati huo huo wazee hao wameshauri kuanzishwa kwa utaratibu wa kulipwa mafao kwa wazee ambao hawakuwahi kuwa katika ajira ya serikali na wale wanaolipwa mafao hayo waongezewe kufuatia kupanda kwa gharama za maisha.
Mafao madogo kwa wastaafu, huduma duni za afya ni miongoni mwa changamoto zinazoendelea kuwakumba wazee wanaoishi Tanzania. Huku baadhi yao, hali za maisha zikiendelea kuwa duni kwa sababu hakuna ongezeko la mafao kwa muda mrefu hali inayo sababishwa na ufuatiliaji hafifu wa serikali.
Umoja wa Wastaafu Tanzania
Emmanuel Samara Katibu Mkuu Umoja wa Wastaafu Tanzania amesema wazee waliostaafu zamani bado wanapata mafao madogo ambayo kwa muda mrefu hayajaongezwa licha ya gharama za maisha kuendelea kupanda hali inayopelekea kuishi kwa tabu.
“Wapo walio staafu zamani wanapata ile pensheni ya mwezi kiasi kidogo sana na kiasi hicho hakijaongezwa muda mrefu sana toka mwaka 2015, wakati gharama ya masiha imepanda na wao wanapata shida na hakuna anaye zungumza juu ya matatizo yao,” ameongezea kusema Samara.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 Tanzania inakadiriwa kuwa na asilimia 6 ya wazee na kati ya wazee hao wengi wanaishi vijijini ambao wanakabiliwa na changamoto za huduma duni za afya pindi wanapopatwa na maradhi.
Huduma za Afya
Methuselah Magoti amesema huduma za afya kwa wazee ambao wamestaafu sio tatizo bali changamoto wanaipata wazee ambao wanatibiwa kwa msamaha wa serikali mara nyingi wamekuwa wakikosa huduma iliyo bora.
“Suala la matibabu kwa wale ambao tuna kadi za bima ya afya unakuta sio tatizo kubwa sana kwa sababu tunapata huduma kama kawaida lakini zile huduma zinazo patikana kwa kadi ya kupewa tu kama ni wazee hilo kwa kweli ni gumu sana halija tekelezwa.”Alisema Magoti
Waziri Mkuu Mstaafu
Hata hivyo Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema njia rahisi ya kuwasaidia wazee ambao hawakuwa kwenye mfumo wa ajira za serikali ni kuanzisha utaratibu wa kuwalipa mafao kama wananchi walivyopendekeza wakati wa kuandika rasimu ya katiba.
“Hili lilizungumzwa sana na wananchi na haswa kwa wananchi wanaoishi vijijini na walikuwa wamependekeza kwamba hi pensheni ingekuwa hata kwa hawa wazee ambao wamestaafu wakiwa katika kazi zao za binafsi,” alisema waziri huyo mstaafu jaji Warioba
Jaji Warioba ameongezea kuwa ni muhimu kwa serikali kushirikiana na wadau wote, ikiwa ni pamoja na wazee wenyewe, katika kubuni na kutekeleza programu na sera zinazo wasaidia wazee huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuchukua hatua zote zinazofaa ili kuwahakikishia wazee haki zao za kijamii na kibinadamu.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania.
Forum