Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 01:12

Tanzania na India kutumia sarafu zake kufanya biashara badala ya dola


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. April 14, 2022 PICHA: AFP
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. April 14, 2022 PICHA: AFP

India na Tanzania zinatafuta namna ya kuendesha biashara kwa kutumia sarafu zake kutokana na uhaba wa dola duniani.

Mkuu wa maswala ya uchumi katika wizara ya mambo ya nje ya India, Dammu Ravi amesema katika kikao na waandishi wa habari mjini New Delhi kwamba India na Tanzania “zinatafuta namna ya kushirikiana katika biashara kwa kila nchi kutumia sarafu yake, na hili ni swala mojawapo ambalo viongozi wa nchi hizi mbili wamelizungumzia.”

Rais wa India Droupadi Murmu, amekuwa mwenyeji wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye yuko India kwa ziara ya kikazi akiandamana na ujumbe wa ngazi ya juu serikalini.

Taarifa iliyotolewa baada ya ziara ya siku mbili ya rais wa Tanzania Suluhu Hassan, inasema kwamba viongozi hao wawili wameelezea nia yao ya kuimarisha biashara kati ya India na Tanzania kwa kila nchi kutumia sarafu yake.

Taarifa hiyo imesema kwamba “benki kuu ya India imeidhinisha hatua ya kutumia Rupee ya India na shilingi ya Tanzania katika uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.”

Benki kuu ya India imezielekeza benki za biashara za India kufungua akaunti za kupokea shilingi ya Tanzania ili kufanikisha makubaliano hayo.

Viongozi hao wawili vile vile wamekubaliana kuimarisha uhusiano wao na kupanua ushirikiano na kufikia kiwango cha ‘kimkakati’.

Uhusiano huo utaziwezesha Tanzania na India kushirikiana katika maswala ya usalama wa baharini, ulinzi, maendeleo, biashara na uwekezaji, miongoni mwa mengine.

India ni mshirika mkubwa wa kibiashara na Tanzania. India hununua korosho, njegere, parachichi na mazao mengine ya kilimo.

Tanzania iliagiza bidhaa za thamani ya dola bilioni 3.9 kutoka India huku ikiiuzia India bidhaa za kiasi cha dola 2.4 mnamo mwaka 2022/2023.

India ni ya tano kwa kuwekeza nchini Tanzania. Uwekezaji wake umefikia thamani ya dola bilioni 3.7 katika sekta mbalimbali.
India ni mojawapo ya nchi tano zilizo katika mpango wa kuachana na matumizi ya dola ya Marekani.

Nchi nyingine ni Brazil, Russia, China na Afrika Kusini.

Forum

XS
SM
MD
LG