Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 03:46

Maduka Kariakoo yafungwa kufuatia tukio la moto


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea soko la Kariakoo lililopo jijini Dar es Salaam, Tanzania. Picha na Global Publishers TV.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea soko la Kariakoo lililopo jijini Dar es Salaam, Tanzania. Picha na Global Publishers TV.

Maduka katika eneo la biashara la Kariakoo, jijini Dar es salaam yamefungwa Jumatatu kufuatia moto uliozuka Jumapili asubuhi na kuteketeza maduka kadhaa katika eneo hilo maarufu la kibiashara.

Wafanya biashara wa eneo hilo muhimu kiuchumi kwa Tanzania na Afrika Mashariki, wana wasiwasi na mali zao na wameitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kutafuta chanzo cha moto huo.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika, wafanya biashara wa eneo hilo, wamesema wanawasi wasi kuhusu usalama wa mali zao kutokana na kuzuka kwa matukio ya moto ya mara kwa mara katika eneo hilo.

Jumla ya kiwango cha hasara kilichosababishwa na moto huo bado hakijafahamika, umeripotiwa moto huo ulianza majira ya saa kumi na mbili asubuhi katika eneo la Mnadani na kuendelea kuteketeza majengo mengine zaidi ya matano likiwemo jengo la Big Bon ambalo lina ofisi za Benki Kuu ya Afrika (BoA).

Rukia Mwinyi mi miongoni mwa wafanya biashara wa eneo hilo ambao mali zao zimeungua, alisema yeye binafsi amepata hasara kubwa, kwa kuwa akiingiza mzigo mpya katika sehemu yake ya biashara siku moja kabla ya ajali kutokea.

Alisema “jana tumenunua vitu vya milioni sita ambavyo vimeingizwa ndani sasa hasara ni kubwa sana na hasara hii sio kwetu peke yetu hata pia kuna watu ambao wana familia ambao wamekuwa wafanyakazi wetu 22 wote wanategemea hili eneo.

Moto huo ambao umewakosesaha ajira wafanyabiashra hao, serikali imetakiwa kuchunguza na kubaini chanzo cha moto huo.

“Ni muhimu sana tukafahamu, hatuwezi kuwa tunakwenda hivi halafu tunakaa chini tunajiuliza tena hivi sababu ni nini tunakaa tunafunika tu” alisema Joshua Lukonge mkazi wa Dar es Salaam na kuongeza

“miaka mitatu minne inapita moto unawaka tena tunajiuliza nini kilitokea kwahiyo ni muhimu sana serikali kufanya uchunguzi.”

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amevipongeza vyombo vya uokoaji kwa kuudhibiti moto huo na kuwataka wananchi kuacha vitendo vya kuziba njia kati ya jengo moja na jingine hali ambayo inazuia harakati za uokoaji na kufanya iwe vigumu kwa magari ya zima moto kufika eneo la tukio.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG