Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 06:12

Polisi wadaiwa kuua raia kiholela Kenya


Nembo ya shirika la haki za binadamu Human Rights Watch
Nembo ya shirika la haki za binadamu Human Rights Watch

Matokeo ya Utafiti wa Human Rights Watch yanaonyesha kuwa polisi wa Kenya wamewaua raia wasiopungua 21 kiholela kwa kutumia nguvu kupita kiasi katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi tangu Agosti 21, 2018.

Polisi walaumiwa

Polisi nchini Kenya mara nyingi wamekuwa wakituhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi na uvunjifu wa sheria wakati wakitekeleza majukumu yao.

Ripoti mpya iliyochapishwa Jumatano na Shirika la haki za binadamu Human Rights Watch limegundua kuwa polisi walikuwa wamehusika katika mauaji ya watu wasiopungua 21 tangu Agosti 2018, katika maeneo mawili ya makazi yasiyo rasmi nchini Kenya.

Vipi Isaac alipoteza uhai wake?

Mnamo Aprili 28, 2017 jioni, Isaac Kamau Mwangi aliondoka nyumbani kwa mama yake katika kitongoji cha Kayole mjini Nairobi kwenda kuchukua gari lake katika eneo la kuosha magari.

Dada yake Ruth Mumbi anasema hizo ndio zilikuwa saa za mwisho kuwa hai.

"Alikuwa amepiga magoti akiwaomba watu waliokuwa wanataka kumuua," Mumbi amesema, akielezea kile mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo alichowaambia familia. "Kitu pekee ambacho mwendesha bodaboda alichosikia ni mlio wa risasi na ndugu yangu akipiga kelele, akiita jina langu. Nikaja kufahamu siku ya pili kwamba alikuwa ameuawa na maafisa wa polisi."

Familia ya Kamau

Rafiki zake wanamkumbuka Kamau kuwa ni mtu aliyekuwa anafanya kazi yake ya udereva wa teksi kwa bidii, na familia inamkumbuka kama baba aliyekuwa anawapenda watoto wake wawili. Kwa polisi, yeye alikuwa ni mhalifu wa kutumia silaha aliyekuwa anatafutwa na polisi.

Mwandishi wa VOA nchini Kenya ameripoti kuwa halmashauri ya kutathmini utendakazi wa maafisa wa polisi nchini Kenya, IPOA, inaeleza kuwa tangu mwaka jana imekuwa ikichunguza visa 133 vinavyohusiana na matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa maafisa hao.

Matokeo haya ya utafiti kutoka kwa shirika hilo la kimataifa linalofuatilia haki za kibinadamu, yanaonyesha kuwa polisi nchini Kenya mara kwa mara wameshindwa kuzingatia sheria katika ufuatiliaji wa mauaji yanayoripotiwa mikononi mwao, kuchunguzwa na kuwahukumu wale wanaopatikana kuhusika katika mauaji hayo.

Eneo lililoathiriwa na mauaji

Mitaa ya mabanda ambayo yametajwa kuathirika na mauaji haya ni Dandora, Mathare, Eastleigh, na Kayole. Tangia Agosti 21, 2018, Human Rights Watch linaeleza kuwa watu hao 21 kutoka Dandora na Mathare wamepoteza maisha yao mikononi mwa maafisa wa polisi kwa tuhuma kuwa walikuwa wahalifu.

Utafiti huo unaonyesha kuwa shirika hilo liliwahoji watu 35 wakiwemo mashahidi, familia za waathirika, wafanyabiashara katika mitaa hiyo, wahudumu wa hospitali kadhaa jijini Nairobi na wanaharakati wa haki za kibinadamu katika mitaa hiyo iliyotajwa.

Human Rights Watch

Human Rights Watch inanukuu chanzo cha habari katika kikosi cha polisi nchini Kenya chenye taarifa juu ya orodha ya majina ya watu ambao wanalengwa kuuliwa na maafisa wa polisi. Orodha hiyo inajumuisha watu waliofarakana na maafisa fulani wa polisi na vile vile wale wanaojihusisha katika wizi wa kimabavu.

Mojawapo wa visa vinavyotajwa na Human Rights Watch katika utafiti wake ni kwamba Aprili 17,2019, kikundi kinachoaminika kuwa sehemu ya kikosi cha maafisa wa polisi maarufu kwa jina la “The Pangani Six” kiliwaua wanaume watano na mvulana mmoja katika maeneo tofauti.

Tarehe hii, vile vile Human Rights Watch linanukuu mashahidi wawili katika kitongoji cha Mlango Kubwa, kwamba walishuhudia maafisa sita wa polisi wakimkamata kijana wa miaka kumi na saba kwa tuhuma za kuhusika katika wizi, kilichofuatia baadaye, hata baada ya kijana huyo kukiri kutokuhusika katika wizi huo, waliwaona maafisa hao wakimburura nje ya nyumba yake, kumfanya kupiga magoti na kumfyatulia risasi na kumuua hatua chache kutoka katika nyumba yake.

Mazoea ya polisi

Hivi ni baadhi tu ya matukio mengi ambayo utafiti huu unavinukuu kuwa ni mazoea ya maafisa wa polisi nchini Kenya kuwakamata vijana, kisha kuripotiwa kutoweka mikononi mwa maafisa wa polisi na kisha baadaye miili yao kupatikana katika hifadhi za maiti viungani mwa jiji kuu la Kenya.

Afisa Mkuu wa Mawasiliano wa Shirika la Human Rights Watch, Afrika Mashariki, Audrey Wabwire ameieleza VOA Swahili kuwa utafiti huu unajenga picha mbovu ya maafisa wa polisi wanaopaswa kulinda maisha ya wananchi.

Utafiti huu pia umezingatia mauaji mikononi mwa maafisa wa polisi, mauaji yanayofungamana na ghasia za uchaguzi na shughuli za kupambana na ugaidi jijini Nairobi na maeneo mengine ukanda wa kaskazini Mashariki na Pwani ya Kenya.

Polisi hawakujibu tuhuma

Juhudi za kuzungumza na msemaji wa polisi Charles Owino na msemaji wa serikali ya Kenya Cyrus Oguna hazikufua dafu kwani hawakuwa wanapokea simu.

Hata hivyo, halmashauri ya kufuatilia na kutathmini utendakazi wa maafisa wa polisi nchini Kenya IPOA, inaeleza kuwa imekuwa ikifuatilia sababu za mauaji wa watu zaidi ya mia moja, mengine yayo yakiwa yanayowalenga maafisa wa polisi jinsi anavyoeleza mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ann Makori.

Asasi hiyo ya polisi pia imelaumiwa katika ripoti hiyo kwa kushindwa kuisaidia halmashauri hiyo inayofuatilia utendakazi wake.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Nairobi

XS
SM
MD
LG