Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 21:46

Pakistani yamzuia mratibu wa CPJ kuingia nchini


Kamati ya Kuwatetea Waandishi wa Habari CPJ
Kamati ya Kuwatetea Waandishi wa Habari CPJ

Serikali ya Pakistan Alhamisi imemzuia mratibu wa programu ya bara la Asia ya Kamati ya kuwatetea waandishi wa habari (CPJ) kuingia nchini humo na kumlazimisha kurejea Marekani, wakidai alikuwa tayari katika orodha ya watu walipigwa marufuku na Wizara ya Mambo ya Ndani kuzuru nchi hiyo.

Kikundi cha kimataifa cha kupigania uhuru wa habari Ijumaa kimelaani kufukuzwa “kwa siri” kwa Steven Butler kama “ni kupigwa kibao cha uso kwa wale wanaokerwa na kukosekana kwa uhuru wa habari” huko Pakistan.

CPJ imesema katika tamko lake kuwa mamlaka ya uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Allama Iqbal ulioko Lahore ulimkatalia Butler kuingia nchini pamoja na kuwa na visa halali, wakitaja yuko katika orodha ya waliopigwa marufuku iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mkurugenzi mtendaji wa CPJ Joel Simon ametaka maelezo kamili kutoka kwa serikali ya Pakistani.

“Iwapo serikali inapendelea kuonyesha nia yake ya kuwepo uhuru wa habari, ni lazima ifanye uchunguzi wa haraka na uliowazi juu ya suala hili,” amesema Simon. Serikali ya Pakistani hadi sasa haijawajibu CPJ.

Tume Huru ya Haki za Binadamu ya Pakistan imesema imesikitishwa na uamuzi wa serikali kumkatalia Bulter kuingia nchini baada ya kuwasili uwanja wa ndege na imetaka uamuzi huo ufanyiwe tathmini upya.

“Kwa upande mmoja, serikali inadai kuwa inajenga sura nzuri ya Pakistan. Upande wa pili, inamzuia mwandishi wa habari mwenye hadhi ya kimataifa na visa kuingia nchini,” tume hiyo imesema.

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema kuzuiliwa na kurejeshwa Marekani kwa Butler “ni ishara mbaya kuwa uhuru wa kujielezea unaoendelea kukandamizwa nchini Pakistan.” Imetaka uamuzi huo ubadilishwe mara moja.

Butler alikuwa Pakistan kuhudhuria mkutano wiki hii unaojadili hali ya haki za binadamu nchini Pakistan. Amekuwa mara kwa mara anatembelea nchi hiyo kufanya kazi na vyombo vya habari vya nchi hiyo na wanaharakati. Kuzuiliwa Butler kuingia nchini kumekuja wakati wasiwasi juu ya udhibiti wa vyombo vya habari umeongezeka Pakistan, japokuwa maafisa wanadai kuwa hali hiyo imekwisha badilika.

Wakosoaji wamelaumu jeshi lenye madaraka makubwa kwa kuzuia vyombo vya habari kuripoti habari zinazokosoa kuongezeka kwao kuingilia siasa za Pakistani na unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya usalama vilivyotokea wakati wa operesheni za kupambana na ugaidi, hususan katika wilaya za kikabila zilizoko nje ya mji karibu na mpaka wa Pakistani.

Msemaji wa Jeshi Meja Jenerali Asif Ghafoor amerejea kukanusha tuhuma hizo na kusema ni propaganda.

XS
SM
MD
LG