Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:34

Marekani yashindwa kuongeza muda wa vikwazo dhidi ya Iran


Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo
Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo

Marekani imeshindwa Ijumaa kupata ridhaa ya kuongeza muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vinavyofikia ukingoni, kukiwa na uwezekano wa Washington kulazimisha vikwazo vya zamani vya kimataifa dhidi ya Iran kurejeshwa mara moja. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amelikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kwa kushindwa kutekeleza jukumu lake la kuendeleza usalama na amani ya kimataifa.

“Imekataa kuongeza muda wa azimio la marufuku ya silaha dhidi ya Iran ambalo limekuwepo kwa miaka 13 kutoa mwanya kwa taifa linaloongoza kufadhili ugaidi kununua na kuuza silaha bila ya kuwepo masharti ya UN kwa mara ya kwanza katika zaidi ya muongo mmoja,” amesema katika tamko lake.

“Kushindwa kwa Baraza la Usalama kuchukua maamuzi muafaka kulinda usalama na amani ya kimataifa hakukubaliki hata kidogo.”

Azimio la Marekani liliungwa mkono kwa kura mbili – za Marekani na Jamhuri ya Dominica. Russia na China zilipiga kura kupinga hatua ya vikwazo hivyo, na nchi nyingine 11 wanachama wa baraza hawakupiga kura.

Balozi wa Iran katika UN Majid Takht Ravanchi, amesema katika tamko lake kuwa vikwazo vyovyote au masharti yoyote yale yatakayo wekwa na Baraza la Usalama “yatajibiwa kwa hatua kali na Iran na ziko njia nyingi za kukabiliana na hilo.”

Majid Takht Ravanchi
Majid Takht Ravanchi

“Katika historia ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, Marekani haijawahi kutengwa kama hivi leo,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Abbas Mousavi ametuma ujumbe wa tweet Jumamosi.

“Pamoja na safari zote walizofanya, shinikizo waliloweka na ubabe wa kivita, Marekani iliweza tu kuihamasisha nchi ndogo [kupiga kura] pamoja nayo,” Mousavi ameandika, akiongeza kuwa “Jana usiku, diplomasia ya Iran inayofanya kazi, pamoja na nguvu ya sheria ya [mkataba wa nyuklia], imeishinda Marekani kwa mara nyingine katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ofisi ya ublozi wa China katika UN imetuma ujumbe wa twitter kuwa matokeo ya kura hizo “unaonyesha kwa mara nyingine kuwa ubinafsi hauwezi kuungwa mkono, na ubabe hautafanikiwa. Jaribio lolote la kuweka maslahi binafsi juu ya maslahi ya wengi ya jumuiya ya kimataifa yatagonga ukuta.”

Marufuku dhidi ya uuzaji au uhamishaji wa silaha za kawaida kusafirishwa kwenda Iran au kutoka Iran unafikia ukomo ifikapo Octoba 18 chini ya mkataba kamili wa Mpango wa Utekelezaji (JCPOA).

Washington inatahadharisha kuwa kuachiwa Iran huru bila ya masharti yoyote itapelekea kudhoofisha zaidi eneo la Mashariki ya Kati, kuongeza vita na ushindani wa kumiliki silaha katika eneo hilo.

Marekani ilieleza kuwa inaungwa mkono katika Mashariki ya Kati kuendeleza vikwazo na Israeli na nchi za Ghuba ya Kiarabu kama sababu yenye mashiko kwa baraza kuongeza muda wa vikwazo.

Hapo awali, Washington ilitaka hatua zaidi ya kujadidisha bila ukomo vikwazo vya silaha, kuwepo vikwazo zaidi na haki ya kimataifa kuzuia usafirishaji wa silaha. Lakini ilirudi nyuma na azma hiyo mapema wiki hii, na kuwasilisha ujumbe uliorekebishwa unaotaka kuendelezwa kwa vikwazo vya silaha.

“Wajumbe wa Baraza wanajua kinacho endelea juu ya dhamira ya Marekani katika mchezo huu,” amesema Richard Gowan, mkurugenzi wa Kundi la Kimataifa Linaloshughulikia Migogoro (ICS).

“Washington ilitaka kuwasilisha azimio hili ili iweze kudai kuwa ilitoa nafasi kwa diplomasia kabla ya kuweka shinikizo kubwa kurejesha nyuma vikwazo dhidi ya Iran, ili iweze kuua kabisa mkataba wa nyuklia uliofikiwa na Iran wa 2015.

Tamko la “Snapback” ni mchakato ambao utaanzisha upya kurejeshwa vikwazo vya zamani vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Iwapo Marekani itachukuwa utaratibu huu, kutakuwa na utata mkubwa, kwa sababu hili linazihusu nchi zilizosaini mkataba wa nyuklia na Iran, na Washington ilijiondoa miaka miwili iliyopita.

“Ni wazi hivi sasa kwamba hakuna utashi wowote wa shinikizo la Marekani kurudisha nyuma vikwazo vilivyopo dhidi ya Iran katika baraza hilo,” Gowan wa ICG amesema.

“Katika hali yoyote ile, Washington intaendeleza kushinikiza hilo, lakini itegemee kutoaminiwa katika dhamira yao ya vikwazo vipya na wajumbe wengine wa baraza.”

XS
SM
MD
LG