Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 01:10

Maafisa zaidi wa USAGM wasimamishwa kazi


Michael Pack
Michael Pack

Mkuu wa shirika la serikali ya Marekani, USAGM, linalosimamia mitandao ya habari za kimataifa, Michael Pack amewaondoa kazini maafisa wengine kadhaa katika hatua ambayo wawili kati ya waliosimamishwa wanasema ni ulipizaji kisasi.

Katika taarifa iliyotumwa kwa magazeti ya Politico na New York Post, msemaji wa USAGM amesema hatua hiyo inakusudia kurudisha “heshima kwa utawala wa sheria katika maeneo yetu ya kazi” hapa USAGM baada ya uhakiki kuonyesha uchunguzi kwa wageni na waandishi wengine wanaoajiriwa na Shirika hilo kwa mitandao yake mitano, ikiwemo Sauti ya Amerika (VOA), haufanyiki ipasavyo.

Maafisa hao wamepewa likizo ya kiutawala, na hati zao zilizowaidhinisha kiusalama kuajiriwa zimefutwa.

Hata hivyo, afisa wa ngazi ya juu aliyeondolewa, Afisa Mkuu wa Mahesabu Grant Turner, amesema hatua hiyo ni kuadhibiwa kwa kusema wazi juu “ya mwenendo unaokiuka maadili ya uongozi” tangu Pack alipochukuwa madaraka mwezi Juni na ni kuhusu uvunjaji wa sheria ya “Firewall” ambayo inawalinda waandishi wa USAGM na shinikizo lolote la kisiasa.

“Nafikiri huku kwa kweli ni kulipiza kisasi kwa mambo mengi ambayo nimekuwa nikiyaleta katika ofisi kuu,” Turner ameiambia VOA katika mahojiano yake. Amesema sababu zilizotolewa juu ya kuondolewa kwake “hazina hoja.”

Eneo la ofisi na studio za VOA, Washington, DC (Photo: Diaa Bekheet)
Eneo la ofisi na studio za VOA, Washington, DC (Photo: Diaa Bekheet)

David Kligerman, ambaye alitumikia kama mwanasheria mkuu wa USAGM na kabla ya hapo Sauti ya Amerika, pia ameondolewa.

“Kama mtumishi wa serikali wa muda mrefu, nilifadhaishwa na hatua hizi zilizochukuliwa,” amesema katika tamko lake kwa VOA. “Hakuna jumuisho lingine unaloweza kufanya isipokuwa ni kulipiziwa kisasi kwa sababu ya kutekeleza jukumu langu la kikazi katika utaratibu usiohusisha siasa na kuwaambia ukweli wale walioko madarakani.

USAGM hakujibu mara moja maswali yanayohusu tuhuma za ulipizaji kisasi au kuthibitisha ripoti za vyombo vya Habari zinazosema maafisa wengine wanne waandamizi wa USAGM pia wamelazimishwa kuondoka katika mkumbo huu.

Baada ya takriban miaka miwili ya kucheleweshwa kuthibitishwa Pack, ambaye alithibitishwa hatimaye Juni 2020 kuchukua nafasi ya juu kabisa ya USAGM, akimrithi Turner, ambaye alikuwa muda wote anakaimu nafasi hiyo.

Tangu wakati huo, viongozi wa juu wa VOA na mitandao mengine wameacha kazi wenyewe au kuondolewa, ajira mpya na matumizi yamesitishwa, na Pack amezuia maombi ya kuongeza muda visa za waandishi wa kigeni wanaofanya kazi katika shirika hilo.

Wakosoaji wake wanasema hatua hizo zinaonekana utashi wa kisiasa na zinakiuka sheria ambazo zimewekwa kulinda uhuru wa waandishi wa USAGM na kuhakikisha kuwa habari zinazotolewa ziko sahihi, zina mizania na za kina.

Baada ya kuapishwa kuchukua nafasi hiyo, Pack aliwaambia wafanyakazi wa VOA kupitia barua pepe kuwa “anaahidi kikamilifu kuheshimu muongozo wa VOA … na uhuru wa waandishi wetu mashujaa kote ulimwenguni.”

Eliot Engel
Eliot Engel

Mbunge Eliot Engel, mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Nje ya Baraza la Wawakilishi, ambayo ina jukumu la kusimamia USAGM, amesema katika tamko lake kuwa kuondolewa kwa Turner na wengine “ni kitendo cha kulipiza kisasi kinyume cha sheria” na ataomba mkaguzi mkuu wa serikali kufanya uchunguzi.

“Nafahamu kuwa watu kadhaa walioachishwa kazi walikuwa wanajaribu kuufahamisha uongozi wa juu wa taasisi hiyo juu ya uwezekano wa hatua zisizokuwa sahihi au vitendo vinavyo kiuka sheria vilivyofanyika wakati wa miezi ya kwanza ya Bwana Pack kushika nafasi hiyo,” Engel amesema katika tamko hilo.

“Ni jaribio la wazi la kutaka kuficha makosa yake hadi hivi leo na kuwanyamazisha wale ambao inawezekana wanataka kueleza wasiwasi wao juu ya maamuzi yake ya siku za usoni,” tamko hilo lilieleza.

Pack amepangiwa kuhojiwa na kamati ya Mambo ya Nje Septemba 24.

Katika mahojiano yake na vyombo vya habari vya mrengo wa kulia na taarifa za habari, Pack amejieleza kuwa yeye ni mleta mabadiliko anayetaka kuondoa upendeleo wa upande mmoja na uongozi mbaya katika USAGM.

Wiki iliyopita, ofisi yake ilitoa ripoti ambayo ilikuwa siri ya ofisi ya Idara ya utawala wa wafanyakazi wa serikali ikisema taasisi hiyo imefeli kwa miaka kadhaa kutekeleza uchunguzi wa kiusalama kwa waajiriwa wapya, wakiwemo waandishi wa kigeni wanaoletwa kwa sababu ya taaluma yao ya lugha maalum.

Matangazo ya USAGM ambayo yapo katika lugha zaidi ya 60 yanalenga nchi 100 na katika baadhi ya hizo serikali zinakandamiza na kudhibiti uhuru wa Habari.

Wengi wa waandishi wa Habari wa USAGM wanaajiriwa kwa visa ya muda ya J-1 ambayo siku za nyuma imekuwa ikiongezwa muda kwa kuidhinishwa na Mkuu wa USAGM. Lakini mwezi uliopita, Pack ghafla alisimamisha kuwasilisha maombi ya kuongeza muda visa hizo, na USAGM ikisema mchakato wa visa unaangaliwa upya, hatua iliyoleta mkanganyiko kwa idhaa zote za VOA na taharuki na ofisi ya Pack.

Katika barua pepe iliyotumwa Julai 23 kwa wafanyakazi, alisema marejeo ya nyuma ya kuhakiki USAGM yaliofanywa na taasisi nyingine ziligundua “hali mbaya, inayoendelea na utaratibu mbaya usiofanya kazi wa kiusalama katika kuajiri” na kuwa shirika hilo “linafanya kazi na wadau wa serikali kuu kuhakikisha dosari zinachukuliwa hatua stahiki na mara moja.”

Pack anasema ameagiza uchunguzi ufanyike kufuatilia operesheni zote zinazotiliwa mashaka za shirika hilo na kwamba “udhaifu uliogunduliwa unakandamiza uwezo wa shirika hilo kutekeleza ujumbe wake, unaharibu ufanisi na ufanikishaji wa nguvu kazi ya serikali kuu, na unahatarisha usalama wa taifa la Marekani.”

Ofisi yake pia imeeleza sababu za usalama wa taifa katika kutetea mabadiliko ya kuzipitia upya visa za J-1 moja baada ya nyingine.

John Lansing, mteule wa Obama aliyekuwa madarakani kabla ya Pack kuongoza USAGM kuanzia Septemba 2015 hadi Septemba 2019, amesema katika tamko lake Alhamisi kuwa viongozi wanaoondolewa madarakani “ni watumishi wa umma ambao utendaji wao ni uliotukuka na alikuwa na fahari kufanya nao kazi.”

John F. Lansing
John F. Lansing

“Jaribio la Pack kuwachafua si jingine bali ni kupotosha jaribio lake la kubomoa uhuru wa kisheria wa maamuzi ya uhariri wa habari wa VOA ili kuingiza propaganda itakayo upendelea utawala, jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa muongozo wa Bunge la Marekani uliounda VOA na USAGM,” Lansing ameandika.

Katika mahojiano na Turner pia aligusia suala la kinga dhidi ya shinikizo la mahitaji ya uandishi.

Amesema ukiukaji wa sheria ni pamoja na kumpangia kazi kwa muda mhariri anaye simamia viwango vya uandishi, Steven Springer, na sera ya visa za J-1, akisema zinazoenda sambamba na kile nilichokiona kuzuia mitandao kupata mahitaji yao ya kitaaluma.”

Msemaji wa Pack ametetea kuondolewa kwa Turner na wengine katika gazeti la Politico, akisema :

“Tumechukua hatua leo kurejesha heshima na hadhi ya utawala wa sheria katika sehemu ya kazi yetu hapa USAGM. Tutachukuwa hatua zaidi kurejesha utukufu wake wa siku za nyuma.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington DC.

XS
SM
MD
LG