Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 03:05

Biden amteua Seneta Kamala Harris kuwa mgombea mwenza wa urais


Sen. Kamala Harris (Kulia) na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden (Kushoto).
Sen. Kamala Harris (Kulia) na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden (Kushoto).

Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Demokratik Joe Biden, Jumanne alimteua Seneta wa jimbo la California, Kamala Harris, kama mgombea mwenza katika uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba mwaka huu.

Kwa kumteua Harris, Biden aliweka historia kwani ni mara ya kwanza kwa mwanamke mweusi kuwa kwenye tiketi ya kuwania urais kupitia chama kikubwa cha kisiasa cha Marekani.

Aidha ni ishara ya Biden kukiri kwamba wapiga kura weusi watakuwa na nafasi kubwa katika azma yake ya kumshinda Rais Donald Trump anayewania muhula wa pili kwa tiketi ya chama cha Republican.

Vile vile, kwa kumteua Harris, Biden anamkumbatia mtu ambaye alikuwa mpinzani wake Kenya uchaguzi wa awali wa kumtafuta mgombea ambaye angepeperusha bendera ya chama cha Demokratik kwenye uchaguzi huo wa urais.

Seneta Harris, mwenye umri wa miaka 55, ni mmoja wa watu mashuhuri sana ndani ya chama hicho, na alitajwa kama mmoja wa watu ambao wangeteuliwa kuwa wagombea-wenza wa Biden punde tu alipositisha kampeni yake ya kuwania uteuzi wa chama.

FILE - Sen. Kamala Harris, D-Calif
FILE - Sen. Kamala Harris, D-Calif

Anaungana na Biden kwenye kampeni wakati ambapo kuna mzozo wa kitaifa ambao haujawahi kushuhudiwa. Janga la Corona limepelekea vifo vya watu zaidi ya 150,000 nchini Marekani, ambayo ni idadi kubwa zaidi kuliko ilivyo katika nchi nyingine kote duniani.

Biashara zimefungwa huku janga hilo likisababisha kudorora kwa uchumi. Wakati huo huo, maandamano na ghasia zimeshuhudiwa katika miji mbalimbali, Wamarekani wakilalamikia ubaguzi na na ukatili wa maafisa wa polisi.

Hakuna mwanamke ambaye amewahi kuwa rais au makamu wa rais nchini Marekani. Ni wanawake wawili tu ambao wamewahi kuteuliwa na vyama vikuu vya Marekani kuwa wagombea wenza katika historia ya Marekani; Mdemokrat Geraldine Ferraro mwaka wa 1984 na Sarah Palin, wa chama cha Republican, aliyeteuliwa na Marehemu John McCain mwaka wa 2008. Hata hivyo, hawakufanikiwa kushinda.

Rais Donald Trump anaelekea kwenye uchaguzi wa Novemba akiwa na makamu wake, Mike Pence, kama mgombea mwenza.

XS
SM
MD
LG