Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 20:50

Maandamano yapata kichocheo kipya kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi mwengine Atlanta


Askari wa zamani wa Idara ya polisi Atlanta Garrett Rolfe akichukua kipimo cha ulevi kutoka kwa Rayshard Brooks, katika eneo la mgahawa wa Wendy.
Askari wa zamani wa Idara ya polisi Atlanta Garrett Rolfe akichukua kipimo cha ulevi kutoka kwa Rayshard Brooks, katika eneo la mgahawa wa Wendy.

Maandamano ya kupinga ubaguzi na matumizi ya nguvu yanayofanywa na polisi, yalipata shinikizo jipya mwishoni mwa wiki hapa Marekani kufuatia kifo cha Mmarekani mwingine mweusi mjini Atlanta, Georgia.

Tukio hilo limesababisha kuongezeka wito wa kupitishwa sheria kuhusu mageuzi kwenye jeshi la polisi na mfumo wa sheria.

Maelfu ya watu walijitokeza katika miji kadhaa nchini Marekani na kwengineko duniani kudai mageuzi ya haraka katika jinsi polisi inavyofanyakazi ili kuzuia utumiaji nguvu.

Maandamano ya mwishoni mwa wiki yaligubikwa na kifo kingine cha Rayshard Brooks aliyepigwa risasi na polisi mzungu alipokataa kukamatwa nje ya mgahawa wa wendys huko Atlanta ijumaa usiku.

Kulingana na video iliyotolewa na polisi Brooks mwenye umri wa miaka 27 aliyekuwa amelala ndani ya gari lake karibu na dirisha la mgahawa wa Wendy la kuhudumia wateja, alibainika amelewa na polisi alipotaka kumkamata alikataa na wakaminyana kidogo na Brooks alipokuwa anakimbia afisa wa polisi alimfyetulia risasi. Meya wa Atlanta akizungumzia tukio hilo anasema hadhani kulikuwa na haja ya kutumia nguvu hizo zote.

Keisha Lance Bottoms, Meya wa Atlanta, Georgia anasema, “ ingawaje kunaweza kuwa na mjadala ikiwa hali iliyojitokeza ilihitaji matumizi ya nguvu namna hiyo au la. Mimi nina amini kwa dhati kuna tofauti kati ya wakati gani unaweza kufanya hivyo na wakati gani huwezi kufanya hivyo. Siamini katika tukio hili ilikua haki kutumia nguvu za kusababisha kifo.”

Msimamo huo umekua ukielezewa na wachambuzi na wanasiasa wengi pamoja na wanaharakati tangu tukio kutokea wakidai mageuzi kufanyika akiwemo mbunge wa zamani wa Georgia Stacey Abrams.

Stacey Abrams, Mbunge wa zamani wa Jimbo la Georgia, “tunahitaji mabadiliko namna polisi wanavyofanya kazi zao. Jinsi idara za polisi zinavyofanya kazi. Kwa sababu kilichotokea jana kwa Raushard Brooks ni hali ya utumiaji nguvu kupita kiasi na uwamuzi kutokana na kwamba walikua na aibu au wameghafilika hadi kusababisha kifo cha mtu ambae walijua hakua na silaha.”

Tayari kuna zaidi ya miji 15 na baadhi ya majimbo ambayo yamepitisha sharia ya kupunguza utumiaji nguvu wa polisi ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kumkaba koo mtuhumiwa, kupatiwa mafunzo na kutumia njia ya kumshawishi mtu unapomkamata.

Katika bunge la taifa, wabunge wa vyama vya Demokratic na Rebulican wangali wanahitilafiana juu ya aina ya mageuzi yanayohitajika. Hata hivyo kuna baadhi ya warepublican wanaonekana wakiwa tayari kuunga mkono baadhi ya mageuzi. Seneta Mrepublican James Lankford wa Oklahoma anasema anaunga mkono marufuku ya kitaifa ya polisi kumbana mtu koo.

James Lankford Seneta Mrepublican wa Oklahoma, “kumekuwepo na makubalianio ya msingi ya muda mrefu kwamba hakuna haja ya kufikia hali hiyo. Kulikua na maridhiano katika mapendekezo ya 2017 ya kuwataka polisi kote nchini kutotumia mbinu hiyo, na mimi nina dhani sisi hatuna tatizo nalo.”

Wanaharakati kwa upande wao wanataka bajeti za idara ya polisi kupunguzwa ili kusaidia miradi ya kijamii na vijana na wengine wakitaka idara kuvunjwa kabisa na kuundwa mfumo mpya wa kulinda raia.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG