Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 11:35

Waandamanaji duniani waonyesha hasira, sikitiko kufuatia kifo cha George Floyd


Waandamanaji baadhi yao wakiwa wamepiga magoti katika uwanja wa Trafalgar Square mjini London Jumapili, Mei 31, 2020, kulaani kilo cha George Floyd, Mmarekani mweusi aliyekufa mikononi mwa polisi huko Minneapolis, Minnesota, Marekani. (AP Photo/Matt Dunham).
Waandamanaji baadhi yao wakiwa wamepiga magoti katika uwanja wa Trafalgar Square mjini London Jumapili, Mei 31, 2020, kulaani kilo cha George Floyd, Mmarekani mweusi aliyekufa mikononi mwa polisi huko Minneapolis, Minnesota, Marekani. (AP Photo/Matt Dunham).

Maandamano yamefanyika katika miji mbalimbali duniani Jumamosi, ikiwa ni mshikamano wa namna fulani na waandamanaji wa Marekani kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi wakati akiwa mikononi mwa polisi mapema wiki hii.

Balozi za Marekani

Balozi za Marekani katika nchi kadhaa zilikabiliwa na waandamanaji, walioghadhibishwa na kifo cha George Floyd kilichotokea Mei 25. Floyd alifariki baada ya polisi mzungu kuweka goti lake kwenye shingo lake kwa takriban dakika 9. Tukio hilo lilirikodiwa katika video, na Floyd alisikika akimlilia polisi mara kadhaa, "Siwezi kupumua."

Berlin Ujerumani

Huko Berlin Jumamosi, maelfu ya Wajerumani walikusanyika nje ya Ubalozi wa Marekani, wakiimba “Uhai wa Watu Weusi ni Muhimu,” kwa mujibu wa chanzo cha habari Forbes.

Toronto Canada

Maadamano juu ya ubaguzi kwa jumla yaliwaleta pamoja maelfu ya watu Jumamosi huko Toronto, Forbes imeripoti.

Ijumaa, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, akizungumzia kifo cha Floyd, amesema katika Makala ya gazeti la The Washington Post, “Ubaguzi uko. Uko nchini Marekani, lakini pia uko Canada. … Tunafahamu watu wanakabiliwa na mfumo wa ubaguzi, kuegemea upande mmoja na ubaguzi dhidi ya watu weusi bila ya kujitambua kila siku.

Mexico City

Huko Mexico City Jumamosi, michoro na maua yalioandaliwa kwa ajili ya kumkumbuka Floyd yalitundikwa katika senyenge karibu na Ubalozi wa Marekani, kwa mujibu wa taarifa zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii.

Umoja wa Mataifa

Siku ya Ijumaa, Kamishna wa Umoja wa Mataifa juu ya Masuala ya Haki za Binadamu Michelle Bachelet pia alilaani mazingira yaliopeleka kifo cha Floyd, ambapo alisema ni tukio la karibuni “katika mlolongo wa mauaji ya Wamarekani weusi wasiokuwa na silaha yaliofanywa na maafisa wa polisi wa Marekani na watu wengine katika jamii.

“Nimesikitishwa kwamba hivi sasa naongeza jina la George Floyd ikiwa katika orodha ya wengine waliouawa akiwemo Breonna Taylor, Eric Garner, Michael Brown na Wamarekani weusi wengine waliouawa wakiwa hawana silaha kwa miaka mingi katika mikono ya polisi – na wengine kama vile Ahmaud Arbery na Trayvon Martin waliouawa na watu wengine katika jamii,” ameeleza.

Dalai Lama

Kiongozi wa kiroho wa Tibet, Dalai Lama, amesema ameona picha za video ya Floyd akiwa amelala chini huku polisi akimwekea goti lake juu ya shingo yake.

“Kwa sababu ya ubaguzi huu kutokana na rangi ya mtu, mambo kama haya yanafanyika,” amesema wakati wa maombi kupitia tovuti Ijumaa.

“Tunashuhudia katika vituo vya habari, vyombo vya habari, juu ya ubaguzi kwa sababu ya rangi ya mtu au dini siku hizi, halafu kuna mauaji kutokana na ubaguzi, na kuna wengine wanajigamba kwa vitendo hivyo kwa kuweza kumuua mtu.”

Umoja wa Afrika

Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Ijumaa ilitoa kauli kali ambayo ni nadra kutolewa kwa umma juu ya matukio ya ndani ya nchi ya Marekani.

Katika tamko hilo, mkuu wa Tume ya AU, Moussa Faki Mahamat, “alilaani vikali” mwenendo wa polisi katika kesi ya Floyd na kutoa “rambirambi za dhati kwa familia na wapendwa wa Floyd.”

XS
SM
MD
LG